Breaking News

Kijana kizimbani kwa kuoa mwanafunzi wa darasa la sita

Na Israel Mwaisaka, Nkasi.

KIJANA mmoja aitwaye Musa Paulo (17) mkazi wa kijiji cha Kacheche wilayani Nkasi mkoani Rukwa amefikishwa katika mahakama ya wilaya Nkasi kwa kosa la kumuoa mwanafunzi wa darasa la sita Emiliana Kasamya (14)

Akisomewa mashitaka mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Ramadhani Rugemalira  na mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi mkaguzi msaidizi wa polisi Hamimu Gwelo alisema kuwa mtuhumiwa kwa makusudi aliamua kumuoa mwanafunzi huyo huku akijua kuwa anatenda kosa kisheria


Alisema kuwa jeshi la polisi lililpata taarifa za mtuhumiwa kuishi na mwanafunzi huyo wa shule ya msingi Kacheche na ndipo walipoweka mtego na kwenda kumnasa mtuhumiwa huyo akiwa anaishi kindoa na mwanafunzi huyo na kuwa kufanya hivyo amevunja kifungu cha sheria No,4(2) cha sheria ya elimu ya mwaka 78

Mshitakiwa amekana shitaka lake na amerudishwa rumande hadi kesi yake itakapotajwa tena marchi 26 mwaka huu,na dhamana ipo wazi ila amekosa wadhamini

Wakati huo huo kijana mmoja mkazi wa kijiji cha Mtapenda John Chulura (Ras)(35) amefikishwa katika mahakama hiyo kujibu tuhuma zinazomkabili za kulima nusu ekari ya bangi

Mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi, Hamimu Gwelo ameiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa alikutwa anamiliki nusu ekari ya bangi iliyolimwa katika kijiji hicho na kukamatwa na baada ya kuhojiwa ndipo alipofikishwa katika mahakama hiyo

Alisema kuwa mtuhumiwa kutokana na kitendo chake cha kulima bangi amevunja sheria  kifungu namba 12(a) ya madawa ya kulevya ya mwaka 2002 na mtuhumiwa amerudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini hadi hapo kesi hiyo itakapotajwa tena march 23 mwaka huu

No comments