Breaking News

Ijue asili ya Sumbawanga

                   Mwene Antony Kapufi Wangao wa III mjukuu wa Mwene Ngalu

Unapolitaja jina la Sumbawanga nje ya maeneo ya mkoa wa Rukwa, tena kwa mtu ambaye hajawahi kufika, wazi kwamba fikra za mtu huyo zinakwenda moja kwa moja kuhusu uchawi na ushirikina.

Matukio ya ushirikina yaliyokuwa yakiripotiwa kutokea yamefanya Sumbawanga kutizamwa kwa mtizamo hasi, kwamba ni eneo la ajabu ambalo watu hawapaswi kuishi.
Zamani kuwapo kwa baadhi ya matukia fulani yaliyokuwa yakihusisha ushirikina

Matukio hayo yalikuwa yakitokea kutokana na sababu mbalimbali moja wapo ikiwa ni baadhi ya wageni kukiuka taratibu na mila na desturi za wenyeji wa Sumbawanga ambao wana sifa ya ukarimu na upendo wa hali ya juu.

(Kinyume na hayo)  Pia sifa ya kabila la kifipa ni wachapakazi hodari waliojikita katika shughuli za uzalishaji mali kupitia kilimo, ufugaji na uwindaji.

Historia ya neno Sumbu- Wanga na Watawala wake.

Kabla sijaanza kuchambua kwa kina yale yaliyokwaza wenyeji wa mji huo wa kabila la Kifipa na kusababisha kuwaadhibu wale waliokiuka mila na desturi zao, nijielekeze kueleza maana ya neno Sumbu- Wanga sio Sumbawanga kama tulivyozoea kulitamka.

Sumbu - Wanga, maana yake ni tupa uchawi, na lilianzishwa na mtawala mmoja wa zamani wa eneo hilo Mwene Ngalu.
    Makao makuu ya Mwene Ngalu wa kabila la Wafipa yaliyopo mjini Sumbawanga


Sumbawanga ni makao makuu ya mkoani Rukwa, uliopo nyanda za Juu Kusini Magharibi mwa Tanzania, ulioanzishwa mwaka 1972, mkoa huo una makabila mbalimbali ila kabila kubwa na la asili ni Wafipa ambao ndiyo asili ya jina Sumbawanga.

Mji huo ulianzishwa mwaka 1803, chini ya chifu wa kwanza wa Ufipa aliyeitwa Kapufi ambaye alitawala miaka ya 1885.

Katibu wa Mila na Desturi za kabila la Wafipa (Midekawa), Domisian Mtuka (62) anaeleza kwamba Chifu Kapufi wa Kwanza alianza miliki yake ndani ya Ufipa yote na makao yake makuu yalikuwa Kijiji cha Kisumba nje kidogo ya mji wa Sumbawanga.

Mke wake aliitwa Mwene Wakulosi ambaye walijaliwa kupata watoto watatu, wa kwanza wa kiume na wawili waliofuata wa kike ambao ni Mwene Kiatu wa pili aliitwa Mwene Ngalu Chinsi chanfipa’ (jina la utawala) na wa tatu aliitwa Mwene Mwati.

Anaeleza kuwa, Baada ya kifo cha Chifu Kapufi wa Kwanza, miliki ilitawazwa kwa mwanae wa kwanza, Mwene Kiatu ambaye alihamia kijiji cha Lwiche ambako kwa mila na desturi za kiutawala, ukitawazwa kuwa chifu  kwakuwa enzi hizo ilikuwa lazima uhame sehemu unayoishi awali na kwenda kuanzisha kijiji chako kama alivyofanya Mwene Kiatu.

Inadaiwa katika kipindi chake cha utawala wa eneo la Ufipa, chifu Mwene Kiatu hakujaliwa kupata watoto na alipokufa, miliki ilichukuliwa na dada yake, Mwene Ngalu ambaye ndiye mwanzilishi wa Sumbawanga.

Chifu Mwene Ngalu alikuwa mtu mwenye upendo na hakupenda uchafu wa aina yoyote ukiwamo uchawi, hivyo kabla ya kuingia kijiji cha Sumbawanga alichokianzisha, aliwataka wananchi waliomfuata watupe uchafu wote kwenye mto Lwiche pamoja na uchawi kisha waingie wakiwa safi.

Kutokana na imani hiyo watu walitupa uchawi wote na taka nyingine kisha wakaingia kijiji cha Sumbawanga wakiwa wasafi.

Aliyekiuka amri hiyo na kuvuka mto Lwiche kutaka kuingia kijiji kipya cha Sumbawanga alikufa wakati akijaribu kuvuka katika mto huo.

"Hapo ndipo ikawa asili ya Sumbawanga na kijiji kikawa na watu walio wasafi na hakukuwa na matatizo katika utawala wa Mwene Ngalu." anasema Katibu huyo

Mtuka anasema kuwa alipendwa na kila ilipotokea ishara ya matatizo ndani ya Ufipa ilikuwa rahisi kutatuliwa kwa kuwa Chifu Mwene Ngalu aliomba na majibu yalipatikana haraka, hasa kwa imani ya usafi waliokuwa nao.

Hata hivyo, Chifu Mwene Ngalu alijaliwa kupata watoto saba ambao wote aliwazalia katika nyumba yake ya utawala iliyojengwa kwa kipindi cha miaka miwili katika mwaka 1918 hadi 1920 chini ya usimamizi wa Mabruda wa dhehebu la Romani Katoliki ambao walikuwa Wajerumani.

Nyumba hiyo hivi sasa imebomoka na limebaki gofu ambalo kwa nje kuna sehemu ya makaburi yanayotumika kuzika kizazi cha utawala huo, na jambo la ajabu kwenye gofu hilo wapo nyuki waliojenga kwenye pango na wapo kwa muda mrefu tangu kipindi cha uhai wa baadhi ya watawala wa kizazi hicho.

Anataja watoto wa Mwene Ngalu ambao ni Maria wa Ngao, Joseph Kapufi wa Ngao, Thadeo wa Ngao, Teresia wa Ngao, Jacob wa Ngao, Victoria wa Ngao na Antony wa Ngao, ambao baada ya kifo cha mama yao, mtoto wa kwanza Joseph wa Ngao alitawazwa kuwa Chifu wa kizazi hicho na kupewa jina la Joseph wa Ngao-Kapufi wa Pili.

Chifu huyo aliyejaliwa watoto wanne, ambao ni Olanda Joseph, Adolf Joseph, Veneranda Joseph na Yovita Joseph na alipofariki dunia nduguye ambaye ni mdogo wake wa mwisho, Antony wa Ngao alitawazwa mwaka 1989, kuwa Chifu wa Ufipa na kupewa jina la Kapufi wa Tatu.

Kapufi huyo wa tatu, Antony wa Ngao, alitawala ufipa tangu mwaka 1989 hadi Desemba 6 mwaka jana alipofariki dunia na kuzikwa kwenye eneo la makaburi ya kizazi cha utawala huo, karibu na jengo la Mwene Ngalu ambalo hivi sasa limebaki gofu tu.

Katika kipindi cha utawala wake, Chifu Kapufi wa Tatu, alijaliwa kupata watoto watatu ambako mkewe wa kwanza alijaliwa kupata mtoto mmoja wa kike aliyeitwa Ntalu na mke mdogo alijaliwa kupata watoto wawili wa kiume ambao ni Oscar na Apolinary.

Hata hivyo baada ya kifo cha Kapufi wa Tatu, hivi sasa ukoo huo wa kichifu uko kwenye mchakato wa kutafiti mrithi wa kiti hicho.

Aidha, baadhi ya maandiko yaliyohifadhi historia ya Sumbawanga na machifu wake, akinukuliwa msemaji wa familia ya akina Kapufi ambaye kwa sasa ni marehemu, Adolf Joseph aliyekuwa mtoto wa Chifu Joseph wa Ngao wa Pili. 

Alidai wazee wa mji huo (wa zamani) walio hai hivi sasa pamoja na wale wa vijiji vya karibu hushirikishwa  katika mchakato wa namna ya  kumpata mrithi huyo  kwa njia ya kuwashirikisha  kuteua majina kadhaa na kuyachambua kupata anayestahili.

Anafafanua kuwa  jina la mrithi likipatikana sherehe za kumsimika kuwa Chifu wa kabila hilo huanza kufanyiwa maandalizi, na kwa kawaida hufanywa nje ya mji kwa kutengeneza sehemu maalumu ya kumpitishia ambayo huiita 'Mzingo'.
Eneo la Makaburi ya Machifu wa kabila la Wafipa yaliyopo kwenye nyumba ya kale iliyokuwa ikitumika zamani

Moja ya jaribio lake la kwanza ni kuvuka mto Lwiche kwa imani kuwa ni moja ya hatua za kudhihirisha kiwango cha usafi wake kabla ya chifu mtarajiwa kutawazwa.

Baada ya sehemu hiyo kukamilika kutengenezwa chifu mtarajiwa hupitishwa kwa nyuma kuingia kwenye mzingo huo huku akipuliza filimbi tatu, ya kwanza ikikataa kulia hupewa ya pili nayo ikigoma hupewa ya tatu ambayo nayo ikigoma ni dalili kuwa hafai kuwa chifu, hivyo huenguliwa na mchakato wa kumtafuta Chifu mwingine unaanza upya.

Adolf anasema ikiwa filimbi moja au mbili zikilia na moja kugoma watampa utawala wa muda huku wakijiandaa kumtafuta chifu mwingine, kwa imani kuwa filimbi zote lazima zilie kwa sababu ni ishara ya sifa njema za utawala za kiongozi anazopaswa kuwa nazo ndipo apewe mamlaka.

Wakati mchakato huo ukiendelea, wa kumpata mrithi wa kiti hicho, mavazi ya Chifu Kapufi wa Tatu, Antony wa Ngao amepewa Vicent Kafumu ambaye ni mjukuu wa Chifu Mwene Ngalu kwa mzaliwa wake wa kwanza aliyeitwa Maria wa Ngao.

Pamoja na hayo yote pia enzi za utawala wa viongozi hao walitumia silaha mbalimbali ambazo hadi leo baadhi yake zimehifadhiwa ili mtawala ajaye akabidhiwe kwa ajili ya kudumisha mila.

Zana hizo ni upinde (ulapwa), mishale (ncheto), fimbo (wasi), mkuki (ilawa) na chombo cha kubebea mishale (untontowaancheto).

Silaha nyingine ni shanga (inkasi) zinazovaliwa mikononi na shingoni kwa chifu, kiti cha miguu mitatu (kisumbi) na vazi la kujifunga kiunoni na mabegani (seketa) ambayo husukwa kwa pamba.

4 comments:

  1. Mmmmh.......
    swa sawa,lakini mtu ni nini kinamuua anapovuka lwiche.
    kuna nn hadi afe(mechanism).
    kwa mtu wa kuja hawezi akaamini kirahisi tu kuwa hakuna uchawi s'wanga kwani dalili zote za uchawi zaonekana,mfano "pembe zinazotembea hewani zikiwa zinawaka moto"

    NOTE;
    binafsi namwamini Mungu,hakuna chakuhofia ktk nchi ya ugenini

    ReplyDelete
  2. uchawi popote upo ila ukiwa mcha wa mungu hakuna kitu cha kukufanya uamini uchawi, karibu ndugu jamaa na marafiki ktk mkoa wetu wa rukwa/sumbawanga kwa amani wafipa ni watu wa upendo wa hari ya juu sana na imani ya kiromani

    ReplyDelete
  3. S'wanga naipenda sana, uchawi mambo yakale saiz tupo bize na mungu ... Rupia daughter

    ReplyDelete