Breaking News

Bunduki 48, Risasi 764 zakamatwa, Padri ahusika katika Ujangili

JESHI la Polisi mkoa wa Rukwa limekamata bunduki 48 ikiwemo moja inayomilikiwa na Padri wa Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga mkoani Rukwa, aliyokuwa akiitumia kwa ajili ya kufanyia vitendo vya ujangili ndani pori la akiba la Lwafi wilayani Nkasi mkoani hapa.



Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Kamishina Mwandamizi wa Polisi, Jacob Mwaruanda alisema jana kuwa bunduki hizo zilikamatwa kufuatia msako uliofanywa na Polisi kwa kushirikiana na kikosi kazi cha taifa na Askari wa wanyamapori wa pori la Lwafi wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.

Alisema kuwa kati bunduki 48 moja ya kivita aina ya AK47, risasi 764 nyara za serikali ambazo ni mikia sita ya tembo, nyama ya nyati kilo ishirini, miba ya Nungunungu, Ngozi moja ya paka pori na Pembe ya Nsya.

Aidha, miongoni mwa silaha hizo pia ilikamatwa bunduki ya Padri wa kanisa Katoliki jimbo Sumbawanga, Parokia ya kirando mwambao wa ziwa Tanganyika, jina tunalo ambapo bunduki yake ni aina ya rifle yenye darubini inayodaiwa kutumika katika ujangili ndani pori la Lwafi wilayani humo.

Kamanda Mwaruanda alisema kuwa kufuatia msako huo, polisi inawashikilia watu 50 ambao baadhi yao silaha zao wanazimiliki kihalali lakini zinatumika kinyume na utaratibu wa kumilikishwa kwao.

Alisema bado wanahojiwa na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Alitoa muda wa mwezi mmoja kuanzia sasa kwamba watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha mara moja kwenye vituo vya polisi au ofisi za serikali za kijiji kabla operesheni kabambe ya kuwatafuta watu hao haijaanza.

Rukwa na Katavi ni miongoni mwa maeneo ambayo ujangili kuua tembo umeshamiri sana hasa katika mapori ya akiba ya Lwafi na hifadhi ya taifa ya Katavi kutokana meno ya tembo kuonekana kuwa na soko katika mikoa mingine nchini na nchi jirani.

Mhifadhi mkuu wa idara ya ulinzi katika hifadhi ya taifa ya Katavi, Davies Mushi alinukuliwa hivi karibuni kuwa kuwepo kwa soko zuri la biashara haramu ya nyara za Serikali hususani meno ya tembo ni moja ya sababu zinazochangia ongezeko la ujangili katika hifadhi hizo.

"Soko zuri la meno ya tembo lililopo katika mji wa Mpanda(Katavi), Sumbawanga (Rukwa), Tabora na maeneo mengine ya nchi linachangia sana kushamiri kwa ujangili ndani ya hifadhi ya taifa ya Katavi lakini tunajitahidi kufanya doria ndani ya hifadhi na kukabiliana na kasi hii iliyopo ya kuua tembo inayofanya na majangili ambao wengi wao ni kutoka nje ya nchi" alisema Mushi.

No comments