Breaking News

KANDEGE AISAMBARATISHA CHADEMA KALAMBO

MSAADA wa Magari matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ambayo mbunge wa jimbo la Kalambo Josephat Kandege ameutoa kwa vituo vitatu vya afya vya Ngorotwa, Matai na Mwimbi wilaya Kalambo umesababisha wanachama 150 wa Chadema kurudisha kadi zao na kujiunga na CCM. 

 Wanachama waliorudisha kadi ni wale wa Kijiji cha Kilewani, wilayani humo, ambao walifanya hivyo katika mkutano wa hadhara wakati mbunge huyo alipokuwa akihutubia kabla ya kukabidhi magari hayo kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanachama hao walisema lengo lao siyo kushabikia siasa bali kumuunga mkono mtu yeyote anayeweza kuwaletea maendeleo kama alivyofanya mbunge huyo.

 Monica Sichalwe, alisema wameamua kurejea CCM kwa vile wanawake wilayani humo wamenyimwa nafasi ndani ya Chadema.

Awali akiwapokea wanachama hao, Mbunge Kandege alisema wote wanaojeruhiwa na vyama vya siasa wanakaribishwa CCM kwani huko ndiko uliko uhuru wa kweli na demokrasia.


Alisema wanachama hao na viongozi walioamua kurejea CCM wamepokelewa kwa mikono miwili na kamwe hawatajutia uamuzi wao.


Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Kalambo Leopard Mbita alisema wakati huu CCM haipo tayari kuwafumbia macho wanachama na viongozi wake ambao ni tatizo hasa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu, kwani wanaweza kukikosesha ushindi.

Mbunge wa jimbo la Kalambo, Josephat Kandege akizungumza na wananchi wa kata na tarafa ya Mwimbi wilayani Kalambo mkoani Rukwa wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jana kijijini hapo.

No comments