Breaking News

Must wakabidhiwa kambi ya Kianda, sasa kuanzisha Campus Rukwa

TATIZO la ukosefu wa wataalamu wenye sifa katika mikoa ya ukanda wa ziwa Tanganyika inayojumuisha mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma, limeanza kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu baada ya Chuo kikuu cha Sayansi na Tekinolojia cha mkoa wa Mbeya (MUST) kukubali kufungua tawi lake mkoani Rukwa.

Makamu mkuu wa chuo cha Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, Prof Joseph Msambichaka alisema hayo hayo jana wakati akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa majengo ya iliyokuwa kambi ya ujenzi wa barabara ya Kampuni ya Aarsleff- BAM Internatioanl iliyokuwa ikijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga kipande cha kutoka Laela kwenda Sumbawanga mjini chenye urefu kilometa 95.3.

Prof Msambichaka alisema kuwa kuanzishwa kwa sehemu ya chuo kikuu hicho katika mkoa wa Rukwa, kitatoa wigo wa elimu kwa wananchi na mikoa ya ukanda wa ziwa Tanganyika yanayojumuisha mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma hiyo hali ambayo itasaidia kupunguza mahitaji ya watu kwenda mbali zaidi kutafuta elimu ya juu hivyo kuongeza wataalamu kwenye maeneo hayo.

Alisema kuwa chuo hicho kitaanza kwa kutoa mafunzo ya uhandisi ujenzi hasa barabara, lakini baadaye fani kama vile za kufanya utafiti na nyinginezo zitaanza kutolewa hali ambayo itasaidia sana kuongeza upatikanaji wa mafundi sanifu na wahandisi hivyo kwa kiasi fulani kuchangia kupunguza tatizo la kuwa wataala wachache kwenye maeneo hayo.


Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema kuwa hiyo fursa ambayo wananchi wa mkoa wa Rukwa na ile ya jirani, wanapaswa kuichangamkia kwa kupeleka watoto wao shule kwa kuwa huduma ya elimu imesogezwa karibu tofauti na ilivyokuwa hapo awali .

Alisema kuwa ujio wa chuo hicho ni mwafaka kwa kuwa mkoa umekuwa ukiangaika juu ya uanzishwaji wa chuo kikuu ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wake kwa urahisi zaidi ambapo kwa sasa vijana wengi wao wanalazimika kutembea umbali mrefu na kwa gharama kubwa kwenda kutafuta elimu ya juu.
Awali, Kaimu mtendaji mkuu wa kitengo cha changamoto za milenia Tanzania (MCA-T) Salim Sasilo alisema kwa kuwa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika hivyo kambi hiyo ambayo ina eneo la mita za mraba 400,000 imekabidhiwa kwa Must ili kuwezesha watanzania kupata elimu ya juu katika nyanja za uhandisi kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalam ambao watakuwa chachu ya kutunza na kuendeleza miundombinu mbalimbali hapa nchini.


No comments