Breaking News

RAS Rukwa aagiza mkurugenzi kupandishwa kizimbani

                        Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa, Tixon Nzunda (kushoto)

Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa, Tixon Nzunda ameagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kalambo iwapo atashindwa kulipa fedha kiasi cha Sh milioni 16 alizozibadilishia matumizi.


Alisema hayo hivi karibuni wakati wa kikao cha kazi cha Madiwani kinacholenga kuboresha mfumo ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kupitia hamasa ya madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa huo.

Alisema katika ukaguzi wa fedha uliofanyika hivi karibuni katika halmashauri za wilaya imebainika kwamba mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Simon Ngagani ametumia fedha za Saccos ya Watumishi kwa ajili ya matumizi mengine kitu ambacho sio sahihi na hakivumiliki.

"Naagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Kalambo anatakiwa kurejesha fedha za Saccos ya watumishi mara moja tofauti na hivyo afikishwe mahakamani hizi pesa za watumishi sio za kuchezea.....wakurugenzi wa aina hii wanaobadilisha matumizi ya fedha msiwachekee" alisema Nzunda wakati akiongea na madiwani.


       Katikati ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kalambo, Simon Ngagani .

Naye, Mwenyekiti wa Saccos ya Watumishi, John Kiondo alisema mkurugenzi wa halmashauri huyo ametumia fedha zao jumla ya Sh milioni 16,920,470 ambazo ni fedha zilizolipwa kutoka hazina na zinazotokana na makato ya wanachama wao ambao ni watumishi wa halmashauri ya Kalambo.

Alisema kutokana kutolipwa kwa fedha hizo kwa muda mrefu sasa tayari wamemuandikia barua ya kusudio la kumfikisha mahakamani iwapo atashindwa kulipa ndani ya siku 21 kuanzia sasa.

Kiondo alisema kutokana na kukosa fedha hizo kumesababisha usumbufu kutoka kwa wanachama wao ambao ni wastaafu wanaokuwa wakitaka kulipwa stahiki zao na kuachana na Saccos hiyo baada ya utumishi wao kufikia ukomo.

Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu mkurugenzi huyo ili alidai yupo kikaoni hivyo hawezi kuzungumza lolote hadi atakapotoka.


No comments