Diwani S'wanga ataka bajeti ya kutalii.
Diwani wa kata ya Momoka (Chadema) katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Norbert Mgala ametaka fedha iliyotengwa kwa ajili ya mafunzo kwa madiwani kuhusu ukusanyaji mapato ya halmashauri hiyo iongezwe ili waweze kwenda kufanya utalii katika hifadhi za taifa za zilizopo kwenye mikoa ya Kaskazini mwa nchi.
Diwani huyo alitoa hoja hiyo wakati akichangia makadirio ya bajeti ya halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga iliyowasilishwa jana kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika mjini hapa.
Alisema kuwa fedha iliyotengwa kwa ajili ya kuwezesha Madiwani 33 wa Manispaa hiyo kwenda ziara ya mafunzo katika Manispaa ya Iringa juu ya vyanzo vya mapato na mbinu za mpya za ukusanyaji mapato ambayo ni Sh milioni 24,060,000 iongezwe ili waweze kwenda katika mkoa wa Arusha kufanya utalii.
" mheshimiwa mwenyekiti mimi nashauri tuongeze fedha katika safari ya madiwani kwenda mkoani Iringa kwa kuwa hatuwezi kuona wanyama wengi zaidi ya mbega wekundu ambao hata hapa mbizi wapo, ingekuwa vizuri tungeenda mikoa ya Arusha kufanya utalii" alisema Diwani Mgala
Akijibu hoja hiyo, Kaimu Mkurugenzi Saad Mtambule alisema kuwa wamechagua kwenda kujifunza katika Manispaa ya Iringa kutokana fedha waliyonayo, hivyo ni vigumu kwenda sehemu nyingine japokuwa ni muhimu kwa madiwani kujifunza katika maeneo tofauti tofauti.
Katika kikao hicho, baraza hilo limepitisha makadirio ya bajeti ya Sh bilioni 47. 24 zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mwaka ujao wa fedha.
Kaimu Mkurugenzi huyo, alisema kuwa kati ya fedha hizo, jumla ya Sh bilioni 1.2 itatokana na makusanyo ya vyanzo vya ndani vya Manispaa huku fedha nyiñgine zikitoka serikali kuu, wahisani na wadau wengine wa maendeleo.
No comments