Breaking News

Fedha za mfuko wa jimbo zazua jambo Sumbawanga.

Mbunge wa jimbo la kwela, Ignas Malocha akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani la hamashauri ya wilaya ya Sumbwanga, Rukwa.
Baadhi ya Diwani wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wamedai hawaridhishwi na matumizi ya fedha za Mfuko wa jimbo kwa zinatumika kwa misingi ya upendeleo.
Akitoa taarifa ya kambi rasmi ya upinzani, Diwani wa kata ya Lyangalile, Amasa Nguvumali alisema fedha ya mfuko wa jimbo la Kwela mgawo wake uzingatie usawa wa maeneo yote ya jimbo hilo kwani vijiji vyote na kata vina haki ya kunufaika na fedha hizo.

"Tuache upendeleo ni haki ya kila kata na kijiji kunufaika na fedha hizo hasa kipindi hiki ambacho wananchi wameibua miradi ya maendeleo lakini inakwama katika utekelezaji kwa kuwa hawajapokea fedha za kusaidia kutoka mfuko wa jimbo wala Serikali kuu" alisema Nguvumali.

Baada ya kuibuliwa kwa hoja hiyo, mbunge wa jimbo la kwela Ignas Malocha alitaka ufafanuzi ni kata zipi ambazo hazijanufaika na fedha hizo kwa kuwa karibu kata zote zimehudumiwa katika kipindi tofauti tofauti.

Naye, Diwani wa kata ya Mnokola, Gerald Kazonda alisema kuwa kata yake ni miongoni mwa kata ambazo hazijanufaika na fedha hizo, hivyo hoja ya mgawo wa fedha za mfuko wa jimbo kuzingatia usawa wa maeneo yote zina mashiko kutokana miradi iliyoibuliwa na wananchi kushindwa kumalizika kwa kukosa fedha.
Diwani wa viti maalumu kata ya Zimba, Marry Mambwe naye alidai kuwa fedha za mfuko wa jimbo wa wamekuwa wakizisikia tu zikisaidia kuendeleza miradi mingine iliyoibuliwa na wananchi huku kata hiyo ikisahaulika.

Hata hivyo, Mbunge Malocha alisema kuwa kata ya Zimba ni miongoni mwa kata mpya, lakini tayari mfuko wa jimbo huo ulisaidia kumalizia ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi Lwanji wakati huo ikiwa kata moja ya Mtowisa.

Mbunge Malocha alitaka madiwani kurejea katika kumbukumbu kwa kuwa fedha hizo katika awamu ya kwanza ziligusa karibu kata zote na zinasaidia kumalizia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na wananchi baada ya miradi hiyo kukosa fedha za kumalizia.

Aidha, katika kikao hicho cha kupitisha bajeti madiwani hao walipitisha makisio ya makusanyo ya bajeti ya halmashsuri kwa mwaka ujao wa fedha ya Sh bilioni 37.8 ambapo kati ya fedha hizo Sh bilioni 2.3 zitatokana na vyanzo vya ndani huku fedha nyingine zikitoka serikali kuu na kwa wahisani mbalimbali wanaosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

No comments