Breaking News

Chadema Rukwa 'kimenuka' waanza kutimua.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila, kushoto akifurahia jambo kabla kuanza kuzungumza waandishi wa habari jana katika ofisi za Chama hicho.

Mwandishi wetu, Rukwa.

Uongozi wa Chadema mkoa wa Rukwa, umetangaza kuwafukuza wanachama 10 na kumvua madaraka Katibu wa chama hicho Sumbawanga mjini, Pius Nguvumali kwa madai ya kutowasilisha fedha za mchango wa matibabu ya Tundu Lisu, upotevu na uharibifu wa mali za chama hicho.



Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila alisema jana kwamba baraza kuu la mkoa la Chadema lililofanya kikao chake Feb. 3 mwaka huu limekubaliana kuwafuta uanachama watu hao na kumvua madaraka ya ukatibu Nguvumali.

Alisema wananchama saba tayari wamekabidhiwa barua za kuvuliwa uanachama kwa tuhuma za kufanya vurugu na kutoa lugha chafu wakati wa ujio wa mwanyekiti wa Bavicha Taifa Halima Mdee ambaye alifanya ziara ya kujenga na kuimarisha chama mkoani hapa.

Aliwataja wanachama waliotimuliwa kuwa ni Osea Mtega, Adolf Kambala, Judith Ulaya, Reguisi Kisanga, Eden, Lucy Mwangambaku na Vitalis maarufu kama Peoples

Inadaiwa kuwa kundi la vijana hao walileta vurugu kwenye mkutano wa ndani wa Chadema hali iliyoonyesha picha mbaya na walivyoitwa mara kadhaa na viongozi wao ili waeleze ni sababu zipi ziliwasukuma kufanya fujo hawakuwa tayari kutoa ushirikiano.

Malila alisema  uongozi pia umemvua madaraka katibu wao, Nguvumali kwa sababu ya kutowasilisha michango ya wanachadema ya matibabu ya Lisu aliyejeruhiwa kwa risasi kupelekwa kutibiwa nchini kenya na baada kuhamishiwa Ubeligiji.

Hata hivyo, Malila hakufafanua ni kiasi cha cha fedha za matibabu ya Lisu ambacho Nguvumali hakuweza kukabidhi, na kuongeza kwamba ameuza Computer na kuharibu pikipiki vyote mali ya chama hicho.

Akihojiwa na gazeti hili, Nguvumali alisema kuwa kwanza yeye tayari alijiuzulu nafasi yake ya ukatibu tangu Januari 29 mwaka huu, ambapo aliwasilisha barua kwa uongozi wa Chadema mkoa na kanda ameamua kufanya hivyo baada ya kuibuka kundi la viongozi kuanza kuwagawa wanachama na viongozi wengine kwa maslahi yao ya kutaka kugombea ubunge mwaka 2020.

Aidha, akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwake alidai kuwa yeye hakuhusika kupokea mchango wowote wa fedha za michango ya Matibabu ya Tundu Lisu waliohgusika kupokea ni viongozi wengine akiwemo mwenyekiti Malila.

Kuhusu komputa alidai iliibiwa na taarifa ilitolewa polisi na viongozi wote wa mkoa wanajua kuhusu suala hilo, huku pikipiki ni mbovu baada ya kupata nayo ajali hivi karibuni.

Nguvumali alisema kwamba tatizo lililopo ni kwamba tayari baadhi ya viongozi wameanza kugawa watu ili wafanye maandalizi ya kugombea ubunge 2020.

"mimi nimeundiwa zengwe kwa sababu nipo karibu na Aida (Khenan) mbunge wa viti maalum ambaye inasemekana ana nia kugombea jimbo la Sumbawanga mjini ambalo na mwenyekiti huyo anataka kugombea ubunge" alisema.

Aliongeza kuwa watu hao kwa muda mrefu sasa wamekuwa hawana uhusiano mzuri kiasi kwamba mara kadhaa viongozi wa Chadema kanda na taifa wamekuwa wakifika na kutafuta suluhu ya kutokuelewana kwao bila mafanikio.

Kwa upande wake, Mbunge Khenan, alisema yeye hajafanya maamuzi ya kugombea ubunge katika jimbo kwani muda ukifika na kama wana Chadema wakitaka afanye hivyo atagombea  lakini kwa sasa ni mapema kuzungumzia hilo kwa kuwa kanuni na taratibu za chama hiziruhusu.

Aliongeza kwamba yeye hana mahusiano mabaya na kiongozi yoyote ndani ya Chadema katika mkoa huo na amekuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano wa hali na mali pale inapohitajika.

No comments