UJANGILI, UVAMIZI TISHIO LA USTAWI WA WANYAMAPORI HIFADHI YA TAIFA YA KATAVI.
Mussa Mwangoka.
UNAPOZUNGUMZIA mikoa yenye utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali ambazo hazijatumika ipasavyo kwa manufaa ya taifa huwezi kusahau kuutaja mkoa wa Rukwa.
Mkoa huo uliopo kusini magharibi mwa Tanzania, ukipakana na mikoa ya Mbeya, Tabora na Kigoma, pia nchi jirani za Jamhuri za kidemokrasia ya kongo na Zambia.
Pamoja na mkoa huo kuwa na rasilimali na maliasili nyingi kama vile ardhi yenye rutuba kwa matumizi ya kilimo, misitu mikubwa na hifadhi za wanyamapori lakini kumekuwapo na tatizo kubwa ambalo limeshamiri kiasi cha kutishia uhai wa baadhi ya viumbe hai ambavo ni faida kubwa kwa taifa.
Tatizo hilo ni kushamiri kwa ujangili ndani ya hifadhi za wanyapori kunakofanywa na majangili na baadhi ya wananchi waishi maeneo yaliyokaribu na hifadhi ya taifa ya Katavi iliyochini ya TANAPA na Mapori ya akiba ya Uwanda na Rukwa Lukwati yaliyopo mkoa Rukwa.
Sanjari na wananchi hao pia raia kutoka nchi jirani ya Burundi wanadaiwa kuwa vinara wa ujangili katika maeneo ambapo wanadaiwa kutumia silaha za kivita kufanya ujangili hali ambayo inatishia uwepo na ustawi wa wanyamapori katika hifadhi hizo.
Majangili wanaonadaiwa ni kutoka nchi hiyo ni wale wanaoishi waliobaki kwenye makazi ya wakimbizi ya Mishamo na Katumba ambao wenzao walirejeshwa makwao na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika wakimbizi la UNHCR.
Hivi karibuni Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige alifanya ziara ya kikazi katika mkoa huo, pamoja na mambo mengi alishuhudia ujangili huo unavyoathiri ustawi wa hifadhi ya taifa ya katavi, Misitu na mapori ya akiba.
Mhifadhi mkuu wa hifadhi hiyoi, John Galla anasema kuwa katika kipindi cha miaka mitano Majangili 887 walikamatwa na bunduki aina za kivita wakitumia katika uwindaji haramu ambazo ni SMG, G3, AK 47 Rifle na risasi ambazo zote idadi yake ni 4894.
Anasema kuwa pia walikamata Maganda ya risasi za SMG na Rifle 68 na Mitambo sita ya kutengenezea magobore, Magobore 103 Baiskeli 187, Mitego ya Wanyama 48,Fataki 110, Misumeno 135, Mikuki 11, Mapanga 107, Shoka 89,na Majembe 4.
Galla anasema kuwa pia walifanikiwa kukamata Ngozi za Simba 12, Chui 6,meno ya tembo 32, mazao ya misitu 7021,samaki kilogramu 16690, nyavu na ndoano 8324.
”Uwindaji haramu kwa ajili ya biashara na nyama pamoja na nyara za Serikali bado unaendelea ukihusisha wananachi wazawa pamoja na Wakimbizi wa Kambi za Mishamo na Katumba. Meno ya Tembo na nyara zingine zimekuwa zikisafirishwa kuelekea nchi jirani za Rwanda na Burundi kwa kutumia biskeli ,pikipiki , na boti” anasema Galla.
Anaongeza kuwa kumekuwa na ujangili mkubwa katika mapori yanayoizunguka Hifadhi, mfano ni Hifadhi ya misitu ya Msaginya upande wa Kaskazini na Hifadhi ya misitu ya Nkamba upande wa Magharibi pamoja na Pori la akiba la Lwafi, na kufanya majangili hao kuvuka na kuwinda katika eneo la Hifadhi.
Anaeleza kuwa aina ya wanyama ambao majangili hao wamekuwa wakiwawinda ni pamoja na Viboko, Nyati, Pofu, Mamba, Tembo, Nyamela na Pundamilia, Swala, Simba, Chui, Nguruwe pori, Kongoni,Twiga, Fisi, korongo,Palapala, Pongo, Pundamilia, Ngiri, Mhanga na pofu.
Galla anaongeza kwamba changamoto kubwa inayojitokeza kiasi cha kutaka kukwamisha jitihada zao za kupambana na Ujangili ndani ya hifadhi na kwenye mapori ya akiba ni pamoja na maamuzi yasiyo yanayotolewa mahakama za wilayani Mpanda dhidi watuhumiwa na majangili wanaokamatwa na kufikisha mahakamani.
Galla alisema kuwa Kumekuwepo na tatizo la watuhumiwa wa kesi za Wanyamapori kuruka dhamana, na kesi hizo kutopewa umuhimu wa aina yake na mahakama kwa kutoa adhabu zisizolingana na uzito wa kesi au kuwaachiwa kwa kisingizio kuwa ushahidi hautoshelezi.
Anadai kwamba kutokana hali hiyo mara nyingi hupelekea watuhumiwa wa ujangili kurudia mara nyingi kuwinda ndani ya Hifadhi hali inayotishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama katika hifadhi na kuathiri utalii wa ndani na nje na hatimaye kulikosesha taifa kukosa mapato.
“Tumeamua kwamba tukiwakamata watuhumiwa wa ujangili ni vizuri kuwapeleka Sumbawanga, ambako huko ndio tutafungua kesi zao naamini haki itatendeka kwani mahakama za hapa Mpanda zimekuwa hazitendi haki kwetu kwani unakamata majangili na ushahidi unakuwepo na sambamba na vidhibiti lakini siku ya mwisho mtuhumiwa anashinda kesi…. Inashangaza ndio sababu ujangili hauishi na unazidi kushamiri” anasema Galla.
Sambamba na hilo, mhifadhi huyo anaeleza kwamba tatizo jingine linalotishia uwepo wa wanyama katika hifadhi hiyo miaka ijazo iwapo juhudi za maksudi hazitachukuliwa kudhibiti ni uvamizi wa maeneo ya hifadhi ambapo wafugaji wamevamia na mifugo yao na kuendesha shughuli za kiuchumi.
Anasema shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa ni pamoja kugeza eneo la malisho ya mifugo yao, kilimo na kujenga nyumba muda kuharibu misitu kwa kuchoma moto, askari wa wanyamapori wamekuwa wakipambana nao na kukamata mifugo yao lakini wamekuwa wakirejea mara kwa mara katika hifadhi hiyo.
Naeleza kuwa wafugaji hao ni wale waliotimuliwa kwenye hifadhi ya Ihefu na Usangu, hivyo wamekimbilia kwenye hifadhi yenye kilometa za mraba 4,471, ikiwa ni hifadhi ya tatu kwa ukumbwa baada ya Ruaha iliyopo mkoani Iringa na Serengeti Arusha.
Mhifadhi huyo anasema hatua mbalimbali wamekuwa wakichukua ili kukabiliana wimbi la ujangili ndani hifadhi, ambapo moja ya hatua hizo ni kutoa elimu wananchi waliopo vijiji vya jirani vinazunguka hifadhi hiyo na kuwaelimisha umuhimu wa uwepo hifadhi hiyo kwa maendeleo ya taifa.
Licha ya elimu hiyo pia hifadhi hiyo kupitia mpango wa ujirani mwema unaoshirikisha wananchi katika katika kuhifadhi maliasili na kuhakikisha pia wananufaika na hifadhi imekuwa ikichangia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, Mchango wa Hifadhi katika miradi hiyo haizidi asilimia sabini (70%), na kila kijiji husika huchangia kiasi kisichopungua asilimia thelathini (30%) ya mradi, ikiwa ni vifaa kama vile mawe, mchanga, tofali na nguvu kazi.
Katika mpango huu Hifadhi huchangia kama Mdau katika kuboresha huduma za jamii katika vijiji vinavyozunguka ambapo imesaidia ujenzi wa nyumba ya kuhifadhia maiti (mortuary) katika hosipitali ya wilaya ya Mpanda.Ujenzi wa jengo la Utawala Pinda Sekondari,
Uwekaji wa Solar Usevya Sekondari, Uwekaji wa Solar Pinda Sekondari,Uwekaji wa Solar Nsimbo Sekondari,Uchimbaji wa visima viwili virefu Ibindi, Ununuzi wa vifaa vya upasuaji kituo cha afya Karema.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige anasema kuwa ili kudhibiti ujangili katika hifadhi hiyo na mapori ya akiba yanayoizunguka, Wizara ya maliasili na utalii kwa kutambua umuhimu wa hifadhi za taifa katika kuongeza pato la taifa kupitia kwenye sekta ya utalii atahakikisha inaboresha maslahi ya watumishi wake hususani askari wa wanyamapori .
Askari wetu lazima wawe na maadili ya kutosha ….. kwa mfano kuhusu ujangili unaweza kusema wanazidiwa ujanja japo sikubali,lakini vipi kuhusu uchomaji wa mkaa, upasuaji mbao watu wanakaa zaidi ya wiki ndani ya hifadhi na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaotoa vibali vya aina hiyo, nadhani nyie ndio mnatoa vibali vya uharibifu huo…… badilikeni na mimi tajitahidi kuboresha maslahi yenu” anasema Waziri Maige.
Anaugiza uongozi wa mkoa wa Rukwa, kuunda tume ya itayochunguza tuhuza zinazoelekezwa dhidi ya maafisa maliasili wa wilaya na mkoa, wanaodaiwa kutoa vibali vya kwa baadhi ya wananchi kufanya shughuli za kiuchumi ndani ya hifadhi ya Pori la Akiba Uwanda.
“tume iundwe watakaobainika wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria ikiwa pamoja na kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani pia waliovamia misitu na mapori ya akiba ikiwa pamoja hifadhi ya taifa ya katavi waondelewe haraka iwezekanavyo” anasema Waziri huyo.
Nahitimisha Makala haya nikisema kwamba Waziri Maige ameona mapungufu katika utunzaji wa Rasilimali na Maliasili za nchi zilizopo Rukwa, huo ni mfano maeneo mengine nchini wanaokwamisha uendelezaji wa hifadhi hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho ni baadhi ya watendaji wasio waaminifu kwa kutoa vibali visivyo rasmi kwa wawindaji haramu ni vema hatua zaidi zichukulie si tu kuunda tume ambayo siku ya mwisho inakosa meno.
Pia ipo haja kwa wizara yenye dhamana ya maliasili na utalii kuongeza vitendea kazi kwa halmashauri za wilaya kitengo cha Misitu na Wanyamapori ili waweze kukabiliana na Ujangili unaoshamiri kila kukicha, lakini sheria namba 5 ya mwaka 2009 ya wanyamapori ifuatwe ili kudhibiti uvamizi wa wafugaji na ndani ya hifadhi hizo.
Mwisho.


No comments