Mbunge wa jimbo la kwela, Ignas Malocha, yeye na mwenzake Aeshi Hilaly wamesusia kushiriki vikao vya kamati ya pembejeo ya wilaya ya Sumbawanga, picha hii alikuwa akizungumza na wananchi wa jimboni kwake. kuhusu habari hiyo soma chini hapo ili kufahamu nini kimewasibu hadi kuamua hivyo
BAADHI ya wabunge katika mkoa wa Rukwa wamesusia kuhudhuria vikao vya vya kamati ya pembejeo ya wilaya ya Sumbawanga, kutokana kile walichodai maamuzi ya vikao kutoheshimiwa.
Wabunge hao ni Aeshi Hilaly wa jimbo la Sumbawanga mjini na Ignas Malocha ambaye ni mbunge wa Jimbo la Kwela, ambao kwa pamoja wamemtuhumu mkuu wa wilaya hiyo,John Mzurikwao, ambaye ni mwenyekiti wa vikao hivyo kwamba amewapa uwakala baadhi ya watu wasio na sifa ya kuwa mawakala.
Wakitoa msimamo wao kwa waandishi wa habari jana, wabunge hao walidai kuwa awali kamati ya pembejeo ya wilaya ilikutana na kupitisha majina ya mawakala baada ya kufanyika kwa utaratibu wa kuchaguliwa na wananchi.
Inadaiwa kuwa awali mawakala hao walipatikana kwa utaratibu wa kupigiwa kura lakini wamestaajabu kuona baadhi ya majina ya mawakala hao yakienguliwa na mkuu huyo wa wilaya ya kuwaingiza wengine kinyume na utaratibu.
"sisi hatuwezi kushiriki katika vikao vyote vya kamati ya pembejeo ya wilaya kwa kuwa mkuu wa wilaya ameweka watu anaotaka yeye..... sisi ndio tunapata shida tunapokutana na wananchi kero ni pembejeo kila eneo kwa sababu amechagua watu ambao hadi sasa hawajafikisha mbolea kwa wakulima" alisema Mbunge Aeshi.
Aliongeza kuwa kwa mfano kuna baadhi ya kata zikwamo Pito na Ntendo mbolea haijafika hadi sasa, kutokana kupatiwa uwakala watu ambao hawakuchaguliwa na wananchi hivyo kushindwa kusambaza mboleo kwa wakulima wa kata hizo.
"tumemshauri mara kadhaa lakini hataki kutusikiliza, juzi nilikuwa kata ya Kaengesa katika vijiji vya Lyapona na Kitete kote huko kero kubwa ni pembejeo hazijafika na huu ndio msimu wa kilimo tayari umeanza mbolea hakuna sisi inatupa shida kwa wananchi" alisema Malocha.
Malocha aliongeza kuwa iwapo kilimo kitakosa mafanikio msimu huu basi kiongozi huyo anapaswa kuwajibika kwa wananchi kutokana na utaratibu wake alioutumia msimu huu, huku akiongeza kuwa msimamo wao utabaki dhidi ya kiongozi huyo wa wilaya.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana Mkuu wa Wilaya hiyo, Mzurikwao alisema kuwa hana taarifa juu ya wabunge hao kutoa tamko la kutohudhuria vikao hivyo na kuongeza kuwa "Kama wametoa tamko waulize wenyewe.... mimi sijalipata hilo tamko la kwa hiyo niseme wazi sijui lolote".
Mawakala katika ya Sumbawanga mjini na vijijini walikumbwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za pembejeo ya kilimo kupitia mfumo wa vocha, hali iliyosababisha baadhi yao kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kufikishwa mahakamani huku Serikali ikibadilisha utaratibu wa namna ya kuwapata ambapo sasa upatikana kwa kupigiwa kura na wananchi katika vitongoji na vijiji. | |
| | | | | | |
No comments