Katibu Mtendaji wa Rango, Stanley Mshana, akitoa mada katika Mdahalo wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kushirika katika mchakato wa kupata katiba mpya jana katika kijiji cha Majalila wilayani Mpanda WANANCHI wanaoishi vijiji vya tarafa ya Kabungu, jimbo la Mpanda vijijini, mkoa mpya wa Katavi wamekataa hoja ya kuchanga fedha kiasi cha Sh 7000 na kumkabidhi mbunge wao, ili aweze kuwanunulia nakala ya Katiba ya sasa kwa madai kuwa kufanya hivyo kutawafanya wawe watumwa dhidi ya mwanasiasa huyo. Kauli hiyo ya wananchi hao ilikuja baada ya mjumbe wa bodi ya Muungano wa taasisi zisizo za kiserikali (Rango) na mratibu wa masuala ya elimu wa haki za binadamu wilaya ya Mpanda, Suleiman Tumaini kutoa ushauri huo kwa wananchi hao. wakati akitoa mada katika mdahalo wa kuhamasisha wananchi wajitokeze kutoa maoni ya juu ya mchakato wa kupata katiba mpya, ulioandaliwa na Taasisi hiyo chini ya ufadhili na shirika la The Foundation for Civil Society na kufanyika katika shule ya Msingi Mpanda ndogo. Mmoja wa wananchi hao, Milambo Iddy alisema kuwa si sahihi wananchi kuchanga fedha na kumkabidhi mbunge huyo ili aweze kutuletea nakala ya katika kwa kuwa hazitafika kwa wakati kutokana na kuwa na kutumia muda mwingi katika vikao vya bunge, shughuli zake binafsi na chama cha ushirika ukizingatia kwamba yeye ni Mwenyekiti wa vyama vya ushirika vya wakulima wa tumbaku. "Nimesikia mtoa mada anasema kama tunataka nakala za katiba ya sasa, tuchange fedha na kumkabidhi mbunge wetu atununulie na kutuletea...... sasa msimamo wetu ni kwamba hatuko tayari kufanya hivyo kwa kuwa tutakuwa watumwa kwake wa nenda rudi maana ana shughuli nyingi, matokeo yake hizo nakala za katiba hazitatufikia wakati mwafaka...... badala yake tunataka maduka yafunguliwe katika kata na vijiji na kuuza hizo nakala za katiba kama ambavyo bidhaa nyingine zivyonauzwa" Alisema. Iddy aliongeza kuwa wana mahitaji makubwa ya kupata nakala za katiba ya sasa kwani vinginevyo hawataweza kutoa maoni kwa usahihi zaidi wakati tume itakapopita kukusanya maoni ya uundwaji wa katiba mpya kwa kuwa ya sasa ambayo imepigiwa kelele kwamba imepitwa na wakati hawajawahi kuisoma na hawajui mapungufu yake. Kauli hiyo iliungwa mkono na Sudi Kasapa ambaye alisema kuwa pamoja na mahitaji makubwa waliyonayo ya kupata katiba hiyo, lakini kamwe hawezi kuchanga fedha na kumpatia mbunge huyo kwa kuwa hawezi kuzifikisha kwa wakati hivyo wanaweza kukosa fursa ya kusoma kwa makini na kubaini mapungufu yaliyopo lakini zikiuzwa madukani wako tayari kununua. Aidha Kasapa alisema kuwa suala la katiba wasiachiwe wanasiasa pekee kulipigia kelele lakini badala yake ipo haja kwa wananchi hasa vijijini kuelimishwa zaidi umuhimu na faida ya kupata katiba mpya kwa kuwa wengi wao hawajui kitu chochote kuhusu katiba hiyo. Hata hivyo baada ya kugoma kupitishia fedha watakazochanga kwa mbunge huyo,Mjumbe huyo wa Rango aliwataka wananchi hao kumpatia yeye mwenyewe na kisha ataagizanakala za katiba hizo mjini Sumbawanga kisha kuwafikishia kupitia kwa afisa tarafa, hoja ambayo wananchi hao walikubaliana nayo. Naye, Katibu Mtendaji wa Taasisi hiyo , Stanley Mshana, aliwahimiza wananchi hao kujitokeza kwa wingi mara baada ya tume ya kukusanya maoni juu ya katiba mpya itakapoanza kufanya kazi ili waweze kushiriki ipasavyo katika mchakato huo na si kalalamika pasipo kuonyesha ushiriki wao. Alisema kujitoa na kutoshiriki katika utoaji wa maoni ni kujisaliti wenyewe kwakuwa kunaweza kusababisha kuundwa kwa katiba isiyoweza kutatua kwa asilimia kubwa changamoto zilizopo kwenye maeneo yao.
No comments