WAHAMIAJI HARAMU WANASWA RUKWA.
Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Tanzania, Mgnus Ulungi. |
Kamanda wa Uhamiaji wa Mkoa wa Rukwa, Wiulson Bambaganya alimtaja mhamiaji huyo haramu kuwa Desiree Sindaigaya (38), ambaye alikamatwa juzi akiwa anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Katumba baada ya kuingia nchini kinyume cha sheria.
“Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Sindaigaya ambaye awali alikuwa akiishi kihalali kama mkimbizi katika kambi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mpanda, ambaye miaka mine iliyopita kwa hiyari yake alirejea nchini Burundi lakini alirejea tena nchini kupitia njia za panya bila hati ya kusafiria na kuishi katika kambi hiyo ya wakimbizi kinyume cha sheria “ alisema
Kwa mujibu wa Kamanda Bambaganya mhamiaji huyo haramu amerejeshwa jana nchini Burundi kupitia kijiji cha Manyovu mkoani Kigoma .
Kamanda huyo wa Uhamiaji alimtaja muhamiaji haramu mwingine kuwa Mohamed Sheikh Mohamed (44) raia wa Kenya mwenye asili ya nchi ya Somalia anadaiwa kuingia nchini na kuishi bila ya vibali vya kusafiria .
Inadaiwa Mohamed alikamatwa juzi mchana katika eneo la Lwiche mjini Sumbawanga, baada ya kutoroka akiwa amedhaminiwa mjini Mpanda akihofia mkono mrefu wa Serikali kwa kuingia , kuishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria .
Kwa mujibu wa Kamanda Bambanganya, alipohojiwa muhamiaji haramu huyo alikiri kuingia nchini bila kuwa na kibali cha kusafiria na kwamba aliweza kuishi na kufanya kazi ya upishi kwa zaidi ya miezi mitatu katika hoteli moja mjini Mpanda, hadi hivi karibuni alipokamatwa kufuatia taarifa za siri kutoka kwa raia wema
“ Mkazi wa mjini Mpanda aitwaye Ali Nuru alimwekea dhamana ndipo muhamiaji huyo haramu alipotoroka.... basi kufuatia taarifa za siri za raia wema ndipo tulipoweka mtego na kumkamata juzi katika eneo la Lwiche” alisema
Kamanda huyo wa Uhamiaji alisema kuwa muhamiahji huyo haramu anatarajiwa kufikishwa kesho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi iliyopo mijini Sumbawanga .
No comments