Breaking News

UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA BADO TATIZO RUKWA.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya.
IMEELEZWA kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mkoa wa Rukwa, bado ni ya kiwango cha chini kutokana na maeneo mengi kukosa miundo mbinu ya kusambaza huduma hiyo.

Hayo yamo katika taarifa ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Stela Manyanya,waandishi wa habari kuhusiana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Alisema kuwa upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo mengi mkoani humo iko chini ya asilimia 50 kiasi ambacho zinahitajika jitihada za ziada ili kuweza kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo.

Manyanya alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa hususani  maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi hutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji na kuongeza kuwa wilaya ya Nkasi ndio ina kiwango kidogo zaidi cha  upatikana wa huduma hiyo.

Alisema kuwa wilaya hiyo inapata maji  kwa asilimia 42, wakati mji wa Namanyere ambao ni makuu ya wilaya hiyo kuna asilimia 16 pekee  ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama.

Alisema hivi sasa mkoa upo kwenye mpango wa Maendeleo ya  Uboreshaji na Usambazaji wa majisafi na salama kwa kila halmashauri kupitia programu ya ndogo ya maji inayofahamika kama mradi wa Vijiji Kumi.

Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa tayari katika mradi huo, jumla ya visima 22 vya majaribio vimekwisha chimbwa kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo, ambapo mwaka huu pia jumla ya visima 11 vinatarajiwa kuchimbwa ili kuboresha huduma ya maji vijijini.

Katika hatua nyingine alisema kwamba uharibifu mkubwa wa mazingira na vyanzo vya maji unaofanywa na wananchi wake umekuwa ni sehemu ya kuongeza kwa tatizo la uhaba wa maji kwenye mkoa huo.

Alizitaka halmashauri za wilaya kutumia sheria ndogo ndogo zilizopo ili kudhibiti tatizo hilo la wananchi kulima katika vyanzo vya maji hali ambayo itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo muhimu.

No comments