Breaking News

WAKULIMA 300 MPANDA KUNUFAIKA NA HATIMILIKI YA ARDHI YA KIMILA.

Makamu wa rais Dk. Mohamed Gharib Bilal akikabidhi hati ya kimila kwa mmoja wa wakulima wa kijiji cha Ilalangulu hivi karibuni akiwa ziara mkoani Rukwa. habari zaidi soma chini hapo.
WAKULIMA wapatao 300 katika vijiji vya Ilalangulu na Mirumba katika tarafa ya Usevya wilayani Mpanda mkoa wa Katavi, wamepatiwa hatimiliki za ardhi ambazo zitayowasaidia kupata mikopo itakayokuza mitaji yao hivyo kuondokana na umasikini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda, Mhandisi Emmanuel Kalobelo, alisema hayo juzi wakati alipozungumza wa waandishi wa habari mjini Mpanda waliotaka kujua mkakati wa halmashauri hiyo katika kuwasaidia wakulima wa ukanda wa Mpimbwe ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa masoko ya mazao.


Alisema kuwa Halmashauri hiyo katika utekelezaji wa mpango wa urasimishaji (Mkurabita) rasilimali na biashara kwa wananchi wake, hadi sasa urasimishaji huo umefanyika katika vijiji vya Ilalangulu na Mirumba ambapo mashamba 1,049 yamepimwa tangu Novemba mwaka jana na jumla ya wakulima 300 wamepatiwa hati ya kumiliki maeneo yao.


Aliongeza kuwa utaratibu huo unawatoa wananchi masikini kutoka kwenye mfumo mfu na usiotambulika kisheria na kwenda kwenye mfumo rasmi unaotoa usalama wa ardhi ya wananchi na wanaweza kuitumia ardhi yao kupata mikopo kutoka katika taasisi za kifedha.


Mkurugenzi huyo, alisema kuwa hatua ya wakulima hao kupatiwa hati miliki ya ardhi imesaidia kumaliza migogora ya ardhi baina yao na wenzao, pia kilio chao cha muda mrefu cha kufanya kilimo kisicho na tija kwao kwani sasa wakipata mikopo itawasaidia kuwapata kwa wakati pembejeo za kilimo ambazo zitakuwa chachu ya uongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.


Mhandisi Kalobelo, alisema licha ya wananchi hao kupatiwa hati hizo za kumiliki mashamba lakini halmashauri hiyo tayari imeanzisha kituo cha kilimo Mwamapuli, ambacho kitasaidia kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya kilimo unaongezeka katika ukanda huo na wakulima wanapata soko la uhakika la mazao yao.


Alisema katika kuhakikisha soko linapatikana zimetengwa ekari 100 ambazo litajengwa soko la kisasa, maghala makubwa ya kuhifadhia mazao hususasi mpunga, kituo cha habari ambazo kitakuwa na jukumu kuwaelimisha wakulima kuhusu kilimo cha kisasa na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya bidhaa zao.

No comments