Breaking News

Maadhimisho ya utepe mweupe yalivyofana wilayani Nkasi mkoani Rukwa

Mtaalamu wa afya kitengo cha maabara hospitali ya wilaya ya Nkasi, Theophil Chinsi akimsaidia kijana David Bitakama kutoa damu kwa hiari ili kusaidia kuokoa vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua jana kwenye maadhimisho ya siku ya utepe mweupe wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Mratibu wa kitaifa wa taasisi ya Utepe Mweupe Rose Mlay, akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe jana wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Na Mwandishi Wetu
Nkasi.

VITENDO vya watumishi wa Idara ya Afya kukimbia vituo vya kazi, kumechangia kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Nkasi, Dk. Fellister Mango alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya idara ya afya na ustawi wa jamii katika siku ya maadhimisho ya utepe mweupe wilayani Nkasi yayokwenda sambamba na zoezi la hiari la utoaji wa damu kwa ajili ya kusaidia kuokoa vifo vya wakina mama wajawazito.

Imedaiwa kuwa kutokana na kuwepo kwa ukosefu wa watumishi wa idara hiyo, kumesababisha baadhi ya wakina mama wajawazito kujifungua kwenye maeneo yasiyo salama na kusaidiwa na wakunga wasio na ujuzi.

Alisema kuwa vifo vingi vya wajawazito kwenye wilaya hiyo hususani mwambao wa Ziwa Tanganyika, vinatokana na kukosa watumishi wenye sifa ambapo kati ya watumishi 500 waliopo 96 ndio wenye sifa pekee.

Alisema wahudumu wa afya ndio wenye jukumu kubwa sasa la kusaidia kutoa huduma za afya, ambapo sehemu kubwa wamekuwa wakisaidia kuzalisha wajawazito hasa katika maeneo ambayo hayana kabisa wataalamu wenye sifa lakini pia ni magumu kufikika.

Hata hivyo uchunguzi huo pia umebaini kuwa wilaya hiyo nye zahanati 39 kati ya hizo 16 zinaongozwa na wauguzi na nyingine kumi zikiongozwa na wahudumu wa afya hali ambayo inafanya huduma za afya kutolewa kwa kiwango cha chini mno.

Takwimu zinaonyesha kuwa, wajawazito 138 kwa wastani wa 100,000 wakati watoto chini ya miaka mitano ni 245 ambao  wamefariki dunia wilayani humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Awali, Mratibu wa kitaifa wa taasisi ya Utepe Mweupe, Rose Mlay, alisema kuwa ni wajibu wa Serikali kutenga bajeti maalum lenye fedha za kutosha kuhakikisha uwepo wa huduma za dharula za kumuokoa mjamzito na mtoto mchanga wakati wa kujifungua.

Alisema kwamba kituo chenye kutoa huduma za dharula (CEmONC) kinatakiwa kuwa na wodi ya wazazi yenye kutoa huduma kwa ufanisi, ikiwemo chumba cha kujifungulia, chumba cha upasuaji na benki ya damu ili akinamama wanaohitaji, waweze kujifungua kwa njia ya upasuaji na kuongezewa damu.


 Mkurugenzi wa Taasisi ya Evidence for Action Tanzania Craig John, jana akizungumza jambo na mkuu wa wilaya ya Nkasi, Iddy Kimanta jana wakati wa maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe wilayani Nkasi mkoani Rukwa.
Mwanamuziki Starah Thomasi ambaye ni balozi wa Utepe Mweupe Tanzania akitumbuiza na watoto kwenye maadhimisho ya siku ya utepe mweupe jana wilayani Nkasi mkoani Rukwa.


No comments