Breaking News

Majambazi wavamia nyumba ya kulala wageni, waporwa mamilioni ya fedha

Kamanda wa Polisi, mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda
Na Sammy Kisika, Sumbawanga.

WATU wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi  waliokuwa  na bunduki wamevamia  nyumba ya kulala wageni kijiji cha Mtowisa wiliyani Sumbawanga ,mkoa wa Rukwa na kuwapora  wafanyabiashara wa ng'ombe fedha taslimu  zaidi ya Sh milioni 13.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia  jana kijijini hapo  katika nyumba ya kulala wageni ya Kaozya mali ya Leonard Kaozya, mkazi wa Sumbawanga mjini wakiwa katika harakati za kununua ng'ombe kabla ya kuvamiwa majira ya saa tano usiku na majambazi hao.


Taarifa iliyopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa na polisi mkoani Rukwa, inaeleza kuwa usiku huo mara baada ya wafanyabiashara wa kabila Kisukuma  kufika kwenye nyumba hiyo baadaye kuliibuka kundi hilo la majambazi waliofika na kuanza kumwulizia mhudumu wa nyumba hiyo ya  wageni lakini mhudumu huyo alifanikiwa kutoroka na kwenda kujificha katika chumba  kimoja cha nje.

"Walipofika walitukuta baadhi ya watu tumekaa nje na walisema kuwa tupo chini ya ulinzi, walianza kuniulizia mimi lakini waliponikosa wakapaza sauti na kusema kuwa wanahitaji wafanyabiashara hao wa ng'ombe na walipowapata walieleza kuwa wao hawataka kuwaua ila walihitaji fedha walizokuwa nazo". Alisema Andrea Cherehani ambaye ni
mhudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni.

Andrea alisema kuwa baada ya kuona kuwa wafanyabiashara hao hawajitokezi walianza kurusha risasi zinazo kadiriwa kufika 17 kwenye paa za nyumba hiyo kabla ya kuingia kwenye vyumba vya nyumba hiyo kwa lengo la kuwasaka wanunuzi hao wa ng'ombe na kuanza kuwapiga kisha kuwapora fedha zao na kutoweka.

Wafanyabiashara hao walioporwa fedha hizo kama walivyojiorodhesha kwenye kitabu cha wageni katika ni pamoja na Shija Rabandiye ambaye anadaiwa kuporwa zaidi ya Sh milioni 10 Masai Bumado na Bakaga Edward.

"Kulikuwa na mfanyabiashara mwingine alikuwa maetoka nje na alipoingia akenda uani ili akachote maji ya kunywa bombani lakini aliposikia sauti ya wajambazi hao naye alikimbia kwa kupitia mlano wa uani huku akiacha wenzake wakisurubiwa na mmoja wao akipigwa na nondo katika paji la uso baada ya awali kukata kutii amri ya majambazi hao". alisema Andrea

Mganga  wa zamu wa kituo cha afya cha Mtowisa Linus Romani alikiri kuwapokea majeruhi wa tukio hilo ambapo amedai kuwa walialazwa hapo usiku huo kabla ya kuruhusiwa siku iliyofuata na kudai kuwa hali zao zinaendelea vema.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wanadaiowa kutokea katika maeneo jirani ya mpakani mwa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa na Momba mkoani Mbeya ambao wana mahusiano ya kikabila na wafanyabiashara hao wa ng'ombe, hivyo ilikuwa rahisi kufuatilia nyendo zao.

Kamanda wa Jeshi la polis mkoani Rukwa Jacob Mwaruanda  licha kuthibitisha tukio hilo alisema kuwa tayari kikosi cha uchunguzi kimekwenda eneo  tukio tangia juzi mchana na kuahidi kutoa taarifa zaidi baadaye.

Mwisho.

No comments