LIPUMBA AIAMBIA MAHAKAMA: POLISI WALINIPIGA!
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba siku alipokamatwa na polisi. Picha kwa hisani ya hakingowi.com
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, hawakufanya maandamano wala kupata barua ya zuio badala yake alipigwa na polisi.
Prof. Lipumba aliyasema hayo mahakamani hapo jana wakati yeye na washtakiwa wengine waliposomewa maelezo ya awali, mbele ya Hakimu Mkazi, Cyprian Mkeha.
Mawakili wa Serikali, Tumaini Kweka, Joseph Maugo na Mohamed Salum, walidai kesi hiyo imekuja mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Akisoma maelezo hayo, Salum alidai CUF waliandika barua Januari 22, mwaka huu, kwenda kwa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kutoa taarifa ya kufanya maandamano kuanzia Ofisi za CUF Wilaya ya Temeke kwenda Mbagala Zakhiem.
Alidai mshtakiwa wa kwanza, Prof. Lipumba ndiye aliyepanga kuongoza maandamano na baadaye kuhutubia kwenye mkutano wa hadhara uliokuwa ufanyike Viwanja vya Zakhiem.
Aliongeza kuwa, Januari 26, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilijibu barua hiyo na kuwataka wasitishe maandamano kutokana na sababu mbalimbali zilizoelezwa ndani ya barua hiyo.
Baada ya maelezo hayo, Prof. Lipumba alisema barua hiyo ilifika saa 12:30 jioni hivyo hakupata ujumbe wowote kama wamezuiwa kufanya maandamano hayo.
Alisema Januari 27, alifika katika Ofisi ndogo za CUF zilizopo Temeke kuzungumza na maofisa wa chama hicho na baadaye walianza maandamano kuelekea Zakhiem.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ulidai kabla ya maandamano hayo hayajaanza, polisi walitoa onyo la kuwataka wasitishe maandamano na kutawanyika kwani wanachokifanya ni kinyume cha sheria.
Licha ya kutolewa kwa onyo hilo, washtakiwa walikaidi amri hiyo,
kuendelea na maandamano na walipofika eneo la Mtoni Mtongani, walikutana na polisi ambao walitoa ilani ya kusitishwa kwa maandamano hayo lakini waliendelea kukaidi.
Baada ya washtakiwa kukaidi amri ya polisi, waliwakamata, kuwapandisha kwenye gari na kupelekwa Kituo cha Polisi Kati ili kutoa maelezo.
Hata hivyo, baada ya kusomewa maelezo na upande wa Jamhuri, mshtakiwa wa kwanza hadi 29, walikana na kudai hawakukaidi amri hiyo wala kufanya maandamano.
"Hatukufanya maandamano, huo ni uongo mtupu kwanza sikupata hiyo barua, isipokuwa polisi waliamua kutukamata na kutupiga tu," alidai Prof. Lipumba.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa, mshtakiwa wa 30 na 31 walikamatwa katika Viwanja vya Zakhiem wakiwa wamekusanya watu kwa ajili ya kufanya mkutano shtaka ambalo walilikana.
Kweka aliieleza mahakama kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo aliomba ipangwe tarehe ya kusikilizwa.
Baada ya kueleza hayo, upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Twaha Taslima aliomba apatiwe maelezo ya mlalamikaji.
Hakimu Mkeha aliahirisha shauri hilo hadi Juni 4, mwaka huu kwa ajili ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa na kuutaka upande wa Jamhuri kuja na mashahidi wawili.
Hivi karibuni, viongozi wa CUF na wafuasi wao walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka matatu ikidaiwa kosa
la kwanza walilitenda Januari 27, mwaka huu, eneo la Temeke ambapo wote kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko kinyume cha taratibu.
Katika shtaka la pili, inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa, wakiwa katika Ofisi ya CUF karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke bila ya kuwa na uhalali, walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano kwenda Mbagala Zakhiem.
Shtaka la tatu, ilidaiwa siku hiyo ya tukio katika eneo la Mtoni Mtongani, waligoma na kutojali tangazo halali lililotolewa na polisi
likiwataka wasiandamane na kutofanya mkusanyiko usio halali.
Washtakiwa hao ni Shabani Tano (29), Shabani Abdallah (40), Juma (54), Athuman Ngumwai (40), Shaweji Mohamed, Hassan Said (37), Mohamed Ibrahim (31), Allan Ally (53) na Abdina Abdina (47).
Wengine ni Allawi Msenga (47), Abdi Hatibu (34), Abdallah Ally (32), Said Mohamed (40), Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25), Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athuman Said (39), Dickson Leasson (37) na Nurdin Msati (37).
CREDIT: MAJIRA
No comments