Breaking News

MAOFISA UANDIKISHAJI WAPIGA KURA WAONYWA KUTOJIHUSISHA NA SIASA WAKATI WA KAZI

Na Gurian Adolf, Sumbawanga

SERIKALI wilayani Sumbawanga imewataka maafisa uandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura kutoingiza itikadi za kisiasa wakati wa uandikishaji wapiga kura kwani kufanya hivyo kunaweza kuhathiri zoezi hilo na baadhi ya watu wakakosa fursa hiyo kitu ambacho ni kuwakosea haki.
Katibu tawala wilaya ya Sumbawanga, Kisasila Masalu alisema hayo jana wakati akifungua semina ya siku mbili kwa maafisa uandikishaji Manispaa ya Sumbawanga yanayofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo mjini hapa.

‘’ Msiingize siasa katika jambo hili kama mtu ana itikadi zake za kisiasa haziweke kando kwani mkionyesha itikadi zenu kuna baadhi ya watu mtawakatisha tamaa ya kuja kujiandikisha kitu ambacho sio sahihi, pia hakikisheni mnafanya kazi hiyo kwa weledi wa hali ya juu, ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima,maana haitakuwa sawa baadhi ya wapigakura waliofika kujiandikisha wasipoona majina yao kwenye daftali hilo’’……alisema. 

Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Sumbawanga Rozaria Mugissa akiwaapisha maafisa wa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura manispaa ya Sumbawanga.
Alisema kuwa huo ni mfumo mpya wa Biometric Voters Registration(BVR) ambao unatumika kwa mara ya kwanza hapa nchini hivyo wanapaswa kujifunza kwa bidii ili wauelewe ambapo zoezi litakapo anza usiwasumbue na kuharibu kazi hiyo.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi afungue mafunzo hayo mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamid Njovu alisema kwa mafunzo hayo yatafanyika kwa siku mbili ambapo maafisa uandikisha watajengewa uwezo wa namna ya kufanya kazi hiyo.

Alisema ni jukumu lao pia kuhakikisha wanahamasisha ili wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwani huu ni uandikisha mpya kwakuwa unatumika mfumo mpya ambapo vitambulisho vya mpiga kura vilivyotumika katika uchaguzi mkuu uliopita havitatumika.

Naye, Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Sumbawanga Rozaria Mugissa mara baada ya kuwaapisha waandikishaji hao aliwaasa wafanye kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa na kutojihusisha vitendo vyovyote vitakavyosababisha kukwamisha zoezi hilo.

No comments