Breaking News

MAUAJI YA KUTISHA KATAVI...WANANDOA WACHINJWA, KICHWA CHATENGANISHWA NA KIWILIWILI

WATU wawili wanandoa wawili wote wakazi wa Kitongoji cha Makambo  Kata ya Itenka wilayani Mlele Mkoani Katavi wameuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo zao na  kutenganishwa kichwa na kiwiliwili  baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana wakati wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao.

Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari  aliwataja wanandoa hao wawili waliouawa kuwa ni  Seth Mwakalimbwa (65) na Yakoba  Kalulu(48)  wakazi wa kitongoji hicho
Kidavashari alisema jana kuwa tukio hilo la mauaji ya kikatili lilitokea hapo juzi nyakati za usiku  wa manane nyumbani kwa wanandoa hao waliokuwa wakiishi pamoja kama mke na mume

 Alisema kwamba  marehemu  hao wakutwa na mauti hayo wakati wakiwa ndani ya nyumba wamelala ambapo kundi la watu wasiofahamika walivamia nyumba yao na kuwaua kwa kuwakata kata na mapanga mwilini kiasi cha kupoteza fahamu kisha kuwachinja kwa kuwatenganisha kichwa na kiwiliwili.

Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa, Balozi wa eneo hilo, Wilbroad Mahenge   alisema kuwa yeye ndio alibaini kutokea kwa mauaji hayo baada ya kutowaona wanandoa hao kwa siku mbili pasipo kuwa na taarifa yoyote.

Mahenge alisema kuwa kutokana na kutokuwa na taarifa yoyote ukizingatia kwamba pia yeye ni jirani yao, alikwenda katika makazi yao  na alipofika hapo,  alikuta  milango ya nyumba yao iko wazi hali ambayo ilimfanya apate mashaka zaidi

 Aliongeza kwamba  alijaribu kuwaita kwa majina yao lakini hakuna  aliyeweza kuitika   hivyo aliamua  kuingia ndani  ya nyumba  yao  na  ndipo  aliwakuta wakiwa  wamelazwa kitandani  huku   wakiwa wamefariki dunia kwa kuchinjwa shingo zao na kutenganishwa na kiwiliwili

 Baada ya kuona hali hiyo,  Mahenge alitoka nje na kasha alikwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa Serikali ya Kitongoji ambao na wao walitoa taatifa kwa jeshi la polisi ambao walifika kwenye eneo hilo muda mfupi baadaye.

Kamanda Kidavashari alisema  chanzo cha  tukio la mauaji hayo ya kikatili  linahusishwa  na imani  za  kishirikina  na mpaka sasa  hakuna mtu  wala watu  waliokamatwa  kuhusika na tukio hilo lakini polisi inaendelea kuwasaka watu hao.

No comments