Breaking News

RCC RUKWA YARIDHIA KUBEBWA MALOCHA NA KANDEGE, UCHAGUZI MKUU UJAO

WADAU wa Maendeleo mkoani Rukwa wameridhia kwa kauli moja kugawanywa kwa majimbo mawili ya uchaguzi ya Kwela na Kalambo, kutokana na majimbo hayo kukabiliwa na changamoto ya kuwa maeneo makubwa ya kiutawala na Idadi kubwa ya watu sambamba na kukabiliwa tatizo ukosefu wa mawasiliano ya simu na barabara hivyo kutofikika kiurahisi.

Wadau hao wametoa kauli ya kuridhia kugawanywa kwa majimbo hayo jana kwenye kikao cha Kamati ya ushauri wa mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa (RDC) ambacho kiliongozwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Linus Sikainda akiwasilisha taarifa ya kuomba ridhaa kugawanywa kwa jimbo la kwela alisema jimbo hilo kwa sasa linakidhi sifa za kugawanywa zilizowekwa na tume ya taifa ya uchaguzi ambazo ni idadi ya watu ambapo jimbo hilo kwa sasa lina wakazi zaidi 235,000, kuna  Changamoto ya maeneo makubwa ya ukitawala, sambamba na ile ile ya kutokuwa na miundombinu ya barabara na mawasiliano ya simu.
Alisema kuwa katika vikao vya kamati ya ushauri wa wilaya (DCC) na Baraza la Madiwani wameridhia kugawanywa kwa jimbo hilo na kuzaliwa kwa jimbo jipya la Ziwa Rukwa, hali ambayo itawapa fursa wabunge wa maeneo hayo kuweza kuwafikia wananchi wote na kusikiliza kero zao kisha kizipeleka serikalini ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu.

Aidha, katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kalambo, Dk Akilimali Mpozemenye alisema kuwa kama ilivyo kwa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, Kalambo pia wameiomba tume ya uchaguzi kuligawa jimbo la Kalambo ili kuweza kuzaa jimbo jipya la Mambwe.
Mbunge wa jimbo la Kalambo, Josephat Kandege

 Alisema wao pia wanavigezo ambavyo vimewekwa na tume ya uchaguzi vya idadi ya watu, changamoto ya mawasiliano na maeneo makubwa ya kiutawala.

Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Chadema, Kapt mstaafu Mzee Zeno Nkoswe, alisema kuwa kutokana na majimbo hayo kuwa na maeneo makubwa ya kiutawala tume ya taifa ya uchaguzi inapaswa kuyagawa ili kuwapa fursa watawala waweze kuwafikia wananchi wote na kusikiliza mahitaji yao ya msingi na kuhakikisha wanayapata tofauti yalivyo sasa ni vugumu viongozi hao kuweza kuwafikia wananchi wote na kusikiliza kero zao hali ambayo imefanya baadhi ya maeneo kudumaa kimaendeleo kutokana kutofikika kiurahisi.

Naye, Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema kuwa kimsingi ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi, kuna kila sababu kwa tume ya taifa ya uchaguzi kuweza kuyagawa majimbo hayo.

Kugawanywa kwa majimbo hayo kutatoa nafuu kisiasa kwa wabunge wa sasa wa majimbo ya Kwela ( Ignas Malocha) na Kalambo ( Josephat Kandege) wanaogombea tena kuwakilisha majimbo hayo kutokuwa na kazi ngumu katika michakato ya ubunge tofauti kama yasipogawanywa.

No comments