Breaking News

Mbaroni kwa kumuua mtoto wake wa kambo.

                              Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando.

Polisi mkoani Rukwa, inamshikilia Kijana mmoja wa miaka 30 mkazi wa kijiji cha Mao kata ya Mbuluma wilayani Kalambo mkoani hapa kwa tuhuma ya kumyonga hadi kufa mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka miwili kwa madai kwamba hampendi.

Kamanda wa Polisi, mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema jana kuwa kijana huiyo anadaiwa kutenda kosa hilo juzi nyakati za saa 11 jioni baada ya kumchukua mtoto huyo aitwaye Agatha Raphaely na kumpeleka shambani ambako alimnyonga na kuutelekeza mwili wake.
Inaelezwa kwamba baada ya kufanya ukatili huo, mzazi huyo wa kiume aliendelea na shughuli zake pasipo kujali lolote huku ikijulikana kwamba mtoto huyo amepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Hata hivyo, mama yake mzazi aitwaye Anisia Kasiti (22) ambaye alikuwa amekwenda mashine alimuuliza mume wake kwamba mtoto amekwenda wapi lakini hakupewa majibu ya kuridhisha ndipo siku inayofuata alipotoa taarifa katika kituo cha polisi.

Polisi walimkamatwa baba wa kambo wa mtoto huyo, ili waweze kumuhoji kwa kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo mtuhumiwa alisikika akiongea kuwa lazima amuue yule mtoto kwani siyo wake.

Aidha, siku hiyo hiyo nyakati za jioni mwanakijiji aitwaye Aron Mwanambogo aligundua kuwepo kwa mwili wa marehemu Agatha shambani kwa mtuhumiwa ukiwa umelala chali kwenye kijito kilichopo ndani ya shamba hilo.

Kamanda Kyando alisema kwamba baada ya kufanyiwa uchunguzi  wa kitabibu iligundulika kuwa marehemu alikufa kutokana  na kukosa hewa baada ya kunyongwa.

Mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi  kukamilika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

No comments