Breaking News

Mguu wa Twiga wawapeleka jela miaka 60


Mwandishi wetu, Katavi.

Mahakama ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi, imewahukumu kifungo cha jumla miaka 60 jela washtakiwa watatu waliokutwa na hatia ya kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria.

Hukumu hiyo imeitolewa jana na hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Teotimus Swai baada ya kuridhishwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande zote mbili za mashitaka.


Washitakiwa waliohukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja ni Juma Kinanda (66), Saidi Shabani (42) wote wakazi wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora na Rashidi Miraji (64) mkazi wa Inyonga wilayani Mlele.

Awali, mwendesha mashtaka wakili wa Serikali, Jamila Miraji alisema mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja alikamatwa Oktoba 11 mwaka jana nyakati za saa 5:30 wakiwa na mguu wa Twiga kinyume cha sheria za wanyama pori.

Aliieleza mahakama hiyo kwamba washtakiwa walikamatwa na askari wa Tanapa waliokuwa katika doria ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Katavi, ambapo waliwakuta na mguu huo wa Twiga.

Aidha,akitoa hukumu hiyo hakimu Swai alisema ushahidi uliotolewa mahakamani na upande mashitaka pasi na shaka umewatia hatiani watuhumiwa hao kwa mujibu wa kifungu cha 86 (1) (2) (c) ii ya sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.

Vilivyosomwa pamoja kifungu 57(1) 60 (2) na sheria ya kuhujumu uchumi na makosa ya kupanga Sura 200 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, hakimu Swai walitoa nafasi ya kujitetea kwa watuhumiwa ambao waliiomba mahakama isitoe adhabu kali kwao kwa kuwa ni wategemezi, maombi ambayo yalitupiliwa mbali na kuhukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja.

No comments