Breaking News

Mwanafunzi wa darasa la sita abakwa hadi kufa

'
Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kapanga iliyopo kata ya Katuma tarafa ya Mwese Wilaya ya Tanganyika, Veronica Lucas (13) amekutwa akiwa amekufa baada ya kubakwa na watu wasiojulikana na kisha mwili wake kutupiwa kwenye shimo la Kolongo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Benedict Mapujila alisema tukio hilo la mauaji ya kikatili lilitokea juzi nyakati za saa 11 jioni kijijini hapo.
Alisema siku hiyo ya tukio Veronica aliondoka nyumbani kwao kama ambavyo ni kawaida yake kwenda shule kwa ajili ya masomo lakini ilipofika nyakati za jioni hakuweza kurudi nyumbani kwao.
Hali hiyo ambayo iliwafanya wazazi wake wapate shaka kwani marehemu hakuwa na tabia ya kutorudi nyumbani kwao.

Siku iliyofuata wazazi wake walikwenda kufatilia shuleni na hawakuweza kumkuta hali ambayo ilizidi kuwatia wasiwasi zaidi na waliamua kwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji hicho.

Viongozi wa kijiji pamoja na wananchi walianza msako wa kumtafuta binti huyo kutwa nzima ndipo ilipofikia nyaklati za saa 11 jioni saa walikuta mwili wake umetupwa kwenye shimo la kolongo.

Kaimu Kamanda Mapujila alisema mwili huo ulikutwa ukiwa sehemu zake za siri zikiwa zimeharibika vibaya.

Alisema uchunguzi wa kitabibu umebaini kwamba chanzo cha kifo hicho ni kutokana na kubakwa na kisha kuvuja damu nyingi hali iliyosababisha mauti hayo yake.

Alisema kwamba hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa ila polisi inaendelea na msako mkali kwa watu waliohusika tukio hilo la kinyama ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

No comments