Breaking News

Risasi zarindima Machimboni Katavi.



Na Walter Mguluchuma, Katavi

Vurugu kubwa zimetokea katika machimbo ya madini ya dhahabu ya Isumamilomo yaliyopo tarafa ya Nsimbo Wilayani Mpanda hali iliyosababisha walinzi wa mgodi wa machimbo hayo kufyatua risasi kadhaa hewani ili kuwatawanya wachimbaji wenye hasira kali.

Taarifa kutoka katika Machimbo hayo zinadai kuwa vurugu hizo baina ya wachimbaj wadogo wa madini ya dhahabu na walinzi wa mgodi wa machimbo zimesababisha kibanda cha ofisi cha kupimia dhahabu na kile wachokaa walinzi kuchomwa moto.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katav, Benedict Mapujila alisema vurugu hizo zimetokea leo (jana) asubuhi zilizodumu zaidi ya saa moja

Alisema chanzo cha vurugu hizo zilitokana na walinzi wa mgodi huo kumkamata mchimbaji mdogo mmoja wa madini ya dhahabu akiwa na jiwe linalosadikiwa kuwa na dhahabu akiwa na lengo la kulitorosha.

Kaimu Kamanda Mapujila alieleza kuwa baada ya mchimbaji huyo kuwa amekamatwa na walinzi hao inadaiwa walianza kumshambulia kwa kumpiga kitendo ambacho kiliwakasirisha wachimbaji wenzake kwa kile walichodai kuwa imekuwa ni tabia ya walinzi wa mgodi huo kuwapiga wachimbaji.

Kutokana na hali hiyo kundi kubwa la wachimbaji lilijikusanya na kisha waliamua kuvamia banda la walinzi wa mgodi na ofisi ambayo limekuwa likitumika kwa ajili ya kupimia dhahabu na kuliharibu na kisha kulichoma moto na kuliteketeza kabisa kwa moto.

Alisema wakati wachimbaji hao wakichoma banda hilo walinzi wa mgodi huo walifyatuwa risasi hewani lakini wachimbaji hao hawakujali waliendelea kuharibu kibanda hicho bila kujali risasi.
Polisi walifika katika eneo hilo baada ya muda si mrefu na waliweza kufanikiwa kutuliza vurugu hizo licha ya kukuta kibanda na ofisi vikiwa vimeharibiwa vibaya na kuteketea kwa moto .

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Generali mstaafu Raphael Muhuga alifika kwenye eneo hilo na kisha alisikiliza kero mbalimbali walizozitoa wachimbaji hao wa madini ya dhahabu .
Aliwataka wachimbaji hao kufuata tararibu zilizowekwa na serikali kwani kitendo cha wachimbaji kutorosha dhahabu bila kupima kunasababisha Serikali kukosa mapato yatokanayo na machimbo hayo ya dhahabu .

Eneo hilo la machimbo ya Isumamilo limekuwa ni maarufu sasa kwa kipindi cha miezi minne sasa kutokana na eneo hilo kwa kuwa zinapatikana dhahabu nyingi na kuna wachimbaji wadogo wadogo zaidi ya 6000 ambao wametoka katika Mikoa mbalimbali hapa nchini na hasa Kanda ya ziwa na wafanyabiashara wa kununua dhahabu.

No comments