Breaking News

Walimu Manispaa ya S'wanga wachachamaa wakidai haki yao.


Baadhi ya walimu wa shule za msingi katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wameutaka uongozi wa halmashauri ya Manispaa hiyo kuwalipa fedha zao uhamisho haraka iwezekanavyo kama serikali kuu ilivyoagiza.

Walimu hao walisema hayo jana kwa nyakati tofauti mara baada katika ofisi za waandishi wa habari mjini hapa, ambapo walidai tangu wamepewa barua za uhamisho feb 28 mwaka huu hawajalipwa stahiki zao hadi sasa.
Mmoja wa walimu hao, Frank Sabuni alisema tangu walipopewa barua za uhamisho, uongozi wa halmashauri ya manipaa hiyo umekuwa ukiwapiga danadana kuwalipa madai yao yanayofikia zaidi Sh milioni 15.

"Sisi tulichokifanya ni kutimiza wajibu wetu kwa maana kwamba tumeripoti katika vituo vipya vya kazi......sasa tunasubiri Serikali itulipe fedha za kujikimu, mizigo, usafiri na usumbufu kitu ambacho hakifanyiki wakati serikali imeagiza kwamba ukitaka kumhamisha mtumishi uwe umeandaa malipo yake" alisema Ephraem Lyombe.

Aliongeza kwamba uongozi wa halmashauri hiyo umekuwa ukipiga chenga kuwalipa fedha hizo, kitu ambacho walimu hao wanafikiri madai yao yanaweza kuingizwa katika madeni ya muda mrefu ya walimu wote hali ambayo inaweza kusababisha kutolipwa kwa wakati stahiki zao kama serikali inavyoagiza.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hamidu Njovu alikiri walimu hao kudai fedha hizo ambazo zimetokana na uhamisho kutokana na kuwepo kwa ikama ya walimu katika baadhi ya maeneo hasa ya pembezoni mwa halmashauri hiyo.

Alisema uongozi wa halmashauri hiyo tayari umewalipa fedha za usumbufu walimu hao hivyo bado wanadai fedha za kujikimu kwa siku 14 ambazo ni haki yao na watalipwa pindi fedha zitakapotikana baada ya madai hao kuyapeleka serikali kuu.

"Tayari tumewalipa fedha zao za usumbufu, hii issue ya usafiri wakija ofisi kuomba magari tutawapatia ila fedha ya kujikimu itabidi wasubiri hadi tutakapopata fedha kutoka serikali kuu" alisisitiza.

Hivi karibuni Waziri  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alikemea uhamisho usiokuwa wa lazima na kutaka watumishi walipwe fedha zao za uhamisho mara moja pindi wanapohamishwa ili kuepuka kuzalisha madeni yasiyokuwa na tija ambayo malipo yake hayajaidhinishwa na Mamlaka yeyote.

No comments