Agizo la JPM latekelezwa, mbolea sasa kufuru Rukwa
Mkoa wa Rukwa, umepokea jumla ya tani 1536 za mbolea ya kukuzia aina Urea, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilotoa mwanzoni mwa wiki hii.
Rais Magufuli aliagiza kwamba mikoa yote yenye upungufu wa mbolea ikiwemo Rukwa, inapata mbolea hiyo ifikapo ijumaa wiki hii ili kupunguza mahitaji ya mbolea hiyo kutoka kwa wakulima.
Mkaguzi wa mbolea kutoka Mamlaka ya udhibiti wa mbolea nchini, (TFRA) Allan Mariki alisema jana wakati wa zoezi la kupakuwa mbolea hiyo kuwa tani 1536 za mbolea ya Urea na 120 za mbolea ya Dap zimepokelewa na kuhifadhiwa katika maghala ya mawakala na kwenye kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).
Alisema mbolea hiyo imesafirishwa na magari ya jeshi kutoka jijini Dar es salaam na kuiingia juzi usiku mjini hapa, ambapo zoezi la kushusha mzigo huo limefanyika leo huku tani nyingine 150 za mbolea ya Dap zikitarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia sasa.
Aidha, lieleza kushangazwa na takwimu za ofisi ya kilimo mkoa wa Rukwa kudai mkoa huo una mahitaji ya mbolea tani 100,000, kitu ambacho sio sahihi kwa kuwa mahitaji ya mbolea kwa nchi nzima ni tani 120,000 ambazo TFRA imekuwa ikiagiza kwa mikoa yote.
"Takwimu za mkoa katika suala la mbolea hazikuwa sahihi, huwezi kusema una mahitaji ya mbolea tani 100,000 wakati kwa nchi nzima mahitaji yake ni tani 120,000 walipaswa kueleza mahitaji sahihi ya mbolea wanayohitaji" alisema Mariki.
Pia aliongeza kuwa tayari waziri wa kilimo ameagiza mamlaka za mkoa na wilaya kuona uwezekana wa kuongeza faida kwa mawakala kulinga na maeneo wanayopeleka mbolea ili iweze kuwafikia wakulima kwa wakati.
Wakala wa mkoa wa Rukwa, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Ikuwo Shadrick Malila walitoa pendekezo la kuomba katika bei elekezi ambayo serikali imeweka waongeze faida ya Sh 1000 ili wapate faida yenye kukidhi matakwa yao ukilinganisha na umbali wa kuwafikia wakulima katika maeneo ya vijijini.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wa mbolea walidai kuwa mbolea iliyopokelewa katika mkoa huo ni nyingi kiasi kwamba hawana uhakika kama itakwisha katika msimu huu wa kilimo.
Mmoja wa wakulima, Eze Simtowe kutoka wilayani Nkasi mkoani hapa, alisema kwamba kuadimika kwa mbolea kuliwafanya wakate tamaa na kuhofia uzalishaji kupungua katika msimu ujao wa mavuno.
Alisema kwa kuwa mbolea imeanza kupatikana madukani wana matumaini ya kupata mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula na biashara.
Katika msimu huu wa kilimo mkoa wa Rukwa ulikuwa umepokea mbolea ya ruzuku ya kupandia aina ya Dap tani 3,764.6 Kati ya 47,869.6.
Hivyo kuwa na upungufu wa tani 44,122.9, huku mbolea ya kukuzia aina ya Urea ikiwa ni tani 2,599.6 wakati mahitaji ni 49,669 hivyo kuwa na upungufu wa tani 47,069.4
No comments