Breaking News

Madawati ya wateja kudhibiti vishoka Rukwa

Mwandishi wetu, Rukwa.

Wananchi wa vijiji vya Kasanga na Kafukoka wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameliomba Shirika la umeme nchini (Tanesco) kuwasogezea haraka huduma ya madawati ya wateja ili waondokane na  usumbufu wa kutapeliwa na vishoka.
Wamesema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati wa wakizungumza na watumishi wa Tanesco waliotembelea maeneo hayo kwa lengo la kutoa huduma kupitia madawati ya wateja ikiwa ni sehemu ya agizo la Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ambaye alitaka mkoa huo kuanzisha madawati hayo ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa Meneja wa Tanesco Mkoani humo, Mhandisi Herini Mhina, Waziri Dk. Kalemani aliuagiza uongozi wa Shirika hilo Mkoani Rukwa kusogeza ofisi zake karibu na wananchi kupitia madawati ya huduma kwa wateja.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kasanga, Zainabu Kaduma alisema kuwa kuanzishwa kwa madawati hayo itawasaidia kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo na kupunguza kero za kutozwa fedha nyingi na vishoka wakati wa kutekeleza miradi ya umeme vijijini (REA)

"Hawa vishoka wamekuwa wakiwatapeli wateja wanaotaka kuwaunganishia huduma ya umeme kwenye nyumba zao, na wakati mwingine kuwatoza fedha nyingi kuliko uhalisia wa gharama ya kuunganishiwa umeme, hivyo madawati ya kutoa huduma kwa wateja yakifunguliwa itakuwa chachu ya kuepukana na adha hizo" Kaduma.

Naye, mkazi wa Kirando, philipo Ndenje alisema kupitia madawati hayo yamewawezesha kupata huduma kwa haraka kwani kabla ya utaratibu huo iliwabidi wasafiri umbali  mrefu  kupata huduma za Tanesco.
"Madawati hayo yamesaidia kupunguza gharama kwani zamani ilibidi kutumia nauli  kuafata huduma wilayani na kupoteza muda mwingi kufuata huduma.” alisema

Kwa mujibu wa ofisa huduma na mahusiano kwa Wateja Tanesco mkoa wa Rukwa, Lucas Kusare mkoa huo tayari umefungua madawati matano ya kusikiliza na kutoa elimu kwa wananchi katika wilaya za Sumbawanga mjini, Nkasi na Laela.



No comments