Matuta barabara ya Tunduma - Sumbawanga, yamkera Naibu Waziri
Na Mwandishi wetu, Rukwa
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhandisi Atashasta Nditiye amekerwa na wingi wa matuta katika barabara ya Tunduma kuelekea Sumbawanga.
Naibu Waziri huyo alionyesha kukerwa na barabara hiyo jana mara baada ya kuwasili na kupokea taarifa ya mkoa huo ambapo yupo Katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua shughuli za maendeleo.
"Nianze kwa kueleza masikitiko yangu kuhusu barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, ina matuta mengi sana zaidi ya 200 hii ni kero kubwa kwa watumiaji wa barabara.....kama lengo kuweka matuta ni kuzuia ajali za barabarani si sahihi waweke alama za barabarani zitasaidia" alisema
Alisema kuweka matuta kunachangia pia kuharibu kwa miundombinu ya barabara, pamoja na magari hasa pale magari yapokuwa yakipunguza mwendo ili kupita katika matuta hayo ambapo uharibu miundombinu ya barabara hivyo kutodumu pia kwa muda mrefu kama inavyotegemewa.
Naibu Waziri alisema kuwa atawasilisha suala hilo kwa waziri wa ujenzi waone uwezekano wa kutatua changamoto hiyo kwa wanaolalamikia matuta hayo sio wamiliki wa vyombo vya usafiri, madereva lakini hata wananchi pia wakerwa na matuta yalipo katika barabara hiyo kwa madai yanafanya safari kuchukua muda mrefu zaidi.
Mara kadhaa wadau wa maendeleo wa mkoa wa Rukwa, wakiwemo wajumbe wa kikao bodi ya barabara ya mkoa huo, Wamekuwa wakitaka kuondolewa kwa matuta hayo wakitoa sababu kama hizo zilizotolewa na Naibu waziri huyo.
Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Dk. Halfan Haule amewahi kunukuliwa akitaka kuondolewa kwa matuta hayo, ambapo alidai kwamba wamekuwa wakitumia muda mrefu wa saa tano hadi saba kusafiri kutoka Sumbawanga hadi Tunduma umbali wa kilometa 220.
Kitu ambacho bado hakina manufaa kwa watumiaji wa barabara hiyo kwa kuwa hali hiyo ni sawa na ilivyokuwa siku za nyuma wakati ikiwa ni barabara ya vumbi.
Barabara hiyo inakadiriwa kuwa na matuta zaidi ya 1000 na yamekuwa yakilamikiwa na watumiaji wake.
No comments