Breaking News

RC ataka waliovamia misitu kusakwa.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mazingira ya REMSO mzee Zeno Nkoswe akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, kuhusu uharibifu wa mazingira uliofanywa katika msitu wa asili wa malangali mjini Sumbawanga.

Mwandishi wetu, Rukwa.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo ameagiza kusakwa na kufikishwa mahakamani kwa watu wapatao 50 waliovamia na kufanya shughuli za kibinadamu katika msitu wa Malangali uliopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Agizo hilo alilitoa jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Malangali muda mfupi baada ya kukagua msitu huo, ambapo watu hao walivamia kwa madai kuwa lilikuwa ni eneo la wazazi wao kabla ya operesheni ya kuanzisha vijiji vya ujamaa iliyofanyika nchi nzima mwaka 1974.

Katika msitu huo, kuna kundi kubwa la watu wamevamia na kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kujenga nyumba,kufuga,kukata miti kwaajili ya kuni,kuchoma mkaa pamoja na kulima kwa madai kuwa eneo hilo ni lao kwani wazazi wao wakati wanaondolewa hawakulipwa fidia.

Msitu huo wenye ukubwa wa eneo la hekta 278, ulitengwa na serikali kwaajili ya kuwa msitu wa asili na kupiga marufuku mtu yoyote kufanya shughuli zozote lakini baadhi ya watu walirudi na kwenda kufungua kesi mahakamani ambapo mahakama iliamuru wahame na waondoke katika msitu huo.

Licha ya amri hiyo ya mahakama watu hao walikaidi na kuendelea na shughuli zao wakiwa na msimamo kuwa wamerejea kwenye eneo lao la asili kwani wazazi wao hawakulipwa fidia hivyo hawaoni sababu za kuondoka na wanaendelea na shughuli za kibinadamu.

Hivi karibuni, wanaharakati wa mazingira walioongozwa na taasisi ya Kaengesa Environment Consarvation(KAESO) pamoja na tasisi ya  Rukwa Environment Management Society(REMSO) walimlalamikia mkuu huyo wa mkoa kuhusu watu hao kuvamia na kuharibu msitu huo ambao ulihifadhiwa kwa lengo la kuhifadhi mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya wanamazingira hao mkurugenzi wa tasisi ya REMSO, Zeno Nkoswe alimweleza mkuu huyo wa mkoa, watu hao wanaharibu msitu huo ambao ni wa asili na umehifadhiwa kwa miaka mingi na mahakama imewataka waondoke lakini wamekaidi na wanaendelea na shughuli za kibinadamu.

Mkuu wa mkoa huo, Wangabo aliamua kufanya ziara ya kutembelea msitu huo ambapo aliwakuta baadhi ya watu  wakiendelea na shughuli kanakwamba hajaamliwa kuondoka kitendo kilicho mkasilisha na kuitisha mkutano wa hadhara.

Katika mkutano huo, aliagiza watu wote wanaoishi ndani ya msitu huo na kufanya shughuli wasakwe na wachukuliwe hatua, ambapo alimtaka mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga Hamidu Njovu  kuhakikisha pia wakandarasi wanaokwenda kuchimba kifusi kwa katika msitu huo kwa lengo la kutengenezea barabara za halmashauri hiyo waache mara moja.

Alisema mkurugenzi huyo ahakikishe mashimo yote yaliyopo katika msitu huo yaliyotokana na kuchukua kifusi yafukiwe na ipandwe miti kwani hayupo tayari kuona msitu huo unateketea kwani una manufaa makubwa kwa mji wa Sumbawanga.

Wangabo alisema kuwa kwakuwa tayari mazao waliyolimwa karibu yakomae yasifyekwe ila pindi yatakapo tolewa asiwepo mtu mwingine anayelima katika msitu huo na kuongeza kuwa miti ipandwe ndani ya mazao hayo ili msitu huo uweze kurudi kama ulivyokuwa hapo awali.

No comments