Breaking News

Jaji awaonya wanaotumia vibaya Tehama.


Na Mwandishi wetu, Rukwa.

Wananchi wameonywa kutotumia vibaya maendeleo ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa kukiuka maadili katika jamii na taifa kwa kuwa sheria hazitawaacha wakiwa salama.

Jaji mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa, John Mgeta alisema hayo leo wakati wa kilele cha siku ya sheria nchini, sherehe ambazo zilifanyika kimkoa katika viwanja vya mahakama kuu mjini hapa.
Jaji mfawidhi Mgeta alisema kuwa kukua kwa tekinolojia habari na mawasiliano nchini isiwe chachu ya kushamiri kwa ukiukwaji wa maadili katika jamii kwani kufanya hivyo ni makosa na sheria zitachukua mkondo wake.

"Niwasihi mtumie vizuri Tekinolojia hii ya habari na mawasiliano kwa kuwa ikitumika vibaya kwa kuomba na kupokea rushwa na kuvunja maadili mengine mtajikuta mkiingia matatani  katika mikono ya sheria ya makosa ya kimtandao (Cyber crime)" alisema Jaji mfawidhi Mgeta

Alisema kuwa matumizi ya Tehama kwa mahakama itasaidia sana kwa kurahisha utoaji wa haki kwa wakati kwa kuwa mashauri yanaweza kuendelea kufanyika na ushahidi ukatolewa pasipo mtoa ushahidi kutokuwepo Mahakamani moja kwa moja kwa kutumia tekinolojia ya video.
Alisisitiza kuwa katika matumizi ya Tehama upo ulazima kuzingatia maadili ili utoaji wa haki uwe wenye weledi na sahihi kwa kutotoa siri au nyaraka yoyote kwa mwananchi au mlengwa kabla ya wakati wake.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alitaka wanasheria hao kubadili mfumo ya utendaji kazi kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kupunguza migogoro isiyo na tija katika jamii.

Alisema viongozi wa kiserikali wamekuwa wakitumia muda mrefu kushughulikia migogoro na malalamiko ya wananchi kwamba hawajatendewa haki katika mashauri mbalimbali.

No comments