Breaking News

Milioni moja yafanya aue babu yake


Jeshi la Polisi mkoa wa Rukwa, linawashikilia watu sita akiwemo mjukuu mmoja aliyechukua hongo Sh milioni moja na kuridhia babu yake auawe kwa kupigwa rungu kichwani kutokana na ugomvi wa ardhi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema leo kwamba tukio la mauaji ya mzee huyo aliyefahamika kwa jina la Paul Kisiwa (72) mkazi wa kijiji cha Ng'ongo lilitokea machi 3 nyakati za jioni kwenye kijiji cha Kifinga Kata ya Mtowisa wilaya Sumbawanga.
Taarifa za kina kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na Diwani wa Kata ya Mtowisa, Edger Malinyi, zilieleza kwamba baada ya kuuawa kwa mzee huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM ngazi ya kata alizikwa kinyemela shambani kwake.

Inaelezwa kuwa taarifa za kupotea mzee huyo zilianza kuzagaa ndipo ndugu wa marehemu, majirani  kwa kushirikiana na polisi walianza kuchunguza tukio hilo, ambapo ilipofika machi 8 mwaka huu, watu hao walimbana mjukuu wa mzee huyo aitwaye John Kisiwa (22) ambaye alikiri kushiriki kupanga njama za kumuua babu yake kwa ujira wa Sh milioni moja.

Diwani huyo, alisema kijana huyo alipanga njama ya mauaji hayo na wenzake ambao walikuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na mzee huyo ambaye awali aliwakodisha watu hao shamba la ekari zaidi 15 kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo.

Alisema baadaye aliwanyang'anya shamba hilo na kuamua kufanya shughuli hizo yeye mwenyewe kitendo kilichowauzi watu hao ambao walijikuta wakiingia katika mgogoro wa kugombea eneo hilo, hali ambayo ilisababisha waandae mipango ya kumuua mzee huyo.

Inadaiwa kwamba siku ya tukio la mauaji hayo, watu hao walimvamia mzee huyo akiwa shambani kwake, ambako walimpiga na rungu kichwani ambapo alianguka na kufariki dunia papo hapo.

Diwani Malinyi alisema watu hao walichimba shimo shamani humo na kumfukia ili kupoteza ushahidi hali iliyobainika baada ya mjukuu wake kubanwa na kueleza ukweli hivyo polisi walifukua eneo hilo na kukuta mwili wa mzee huyo.

Kamanda Kyando alisema aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa kuwa ni Kela Lubinza (15), Chani Lubinza (29), Simba Lubinza (16)  wote wa familia moja pia Deshi Mihambo (40) na Muli Sabini (21).

Alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa mara baada ya uchunguzi wa awali utakapokamilika.

No comments