Breaking News

Waziri Ummy amwaga cheche siku ya wanawake Duniani


Mwandishi wetu, Rukwa.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewaonya wakurugenzi wa halmashauri nchini wasiotenga asilimia nne ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya mikopo ya wanawake.

Waziri huyo amesema hayo leo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, yaliyofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela mjini hapa.

Waziri Ummy alisema kuwa wakurugenzi wasiotenga fedha kwa ajili ya mikopo ya wanawake atachukua majina yao na kuyakabidhi kwa Rais John Magufuli ili aweze kuwachukulia hatua za kinidhamu ikiwemo kuwaondoa katika nafasi zao.

"Naagiza wakurugenzi wote wa halmashauri nchini wasiotenga asilimia 4 ya mikopo kwa wanawake waanze kufanya hivyo mara moja, wale watakaobainika nitachukua majina yao na kuyapeleka kwa mheshimiwa Rais ili awafute kazi maana wanakiuka sheria tulizojiwekea" alisema Ummy

Pamoja na kutenga fedha hizo kwa ajili ya mikopo ya wanawake, pia alitaka halmashauri kuacha mara moja kutoa mikopo ya fedha kiduchu kwa wanawake na vijana badala yake watoe fedha ambazo zitawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Awali, Mwakilishi wa Ubalozi wa Canada na kitengo cha Wanawake cha Umoja wa Mataifa, Sue Steffen wakati siku hii ikiadhimishwa wanawake wengi nchi bado wanakabiliwa na changamoto za kunyimwa haki mbalimbali ikiwemo kumiliki ardhi.

Alisema ili wanawake wa vijiji wanapaswa kuwezeshaji kiuchumi, kijamii, kisiasa, na utamaduni, waweze kuondokana na changamoto hizo.
Naye, Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hilaly aliiomba Serikali kuwapatia gari kwa ajili ya kubeba wagonjwa kwa kuwa hospitali na vutuo vya afya mkoani humo vina mahitaji makubwa ya gari hilo.

Alisema kukosekana kwa gari hilo kumesababisha wakina mama wajawazito kupoteza maisha kutokana na kushindwa kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya upasuaji.

No comments