Breaking News

Waziri Ummy Mgeni Rasmi siku ya Wanawake Duniani mkoani Rukwa



Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto, Ummy Mwalimu atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu.

Ikumbukwe kwamba maadhimisho hayo ufanyika  machi nane ya kila mwaka, ambapo kila mkoa inaadhimisha kivyake huku uongozi wa mkoa wa Rukwa, umemwalika Waziri Ummy na kilele chake kitafanyika kesho kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya jamii na jinsia, Julius Mbilinyi amesema leo kwamba kauli mbiu yamaadhimisho hayo ni "kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake wa vijijni".

Alisema uwezeshaji wa wanawake wa vijijini kiuchumi, kijamii, kisiasa, na utamaduni, ni chachu ya kuelekea katika uchumi wa kati wa viwanda.

"Wanawake ndio chachu ya maendeleo ya uchumi wa taifa lolote lile, hivyo sisi kama wizara tunaihamasisha jamii ya kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake hao ili tuweze kufikia malengo" Alisema Mbilinyi

Alisema pia wakiwezeshwa na kujua haki zao na kuweza kuzitetea katika jamii watakuwa na mchango mkubwa katika taifa kwa kuwa watamudu kufanya shughuli za uzalishaji mali ambazo zitawaongezea kipato wao binafsi lakini kukuza uchumi wa taifa.

Awali, Afisa Maendeleo ya jamii mkoa wa Rukwa, Azazi Kalyatila alisema kuwa maadhimisho ya siku ya wanawake yameambatana na wanawake wa mkoa huo kutembelea makundi ya mahitaji maalumu kama shule ya msingi malangali ambako walitoa misaada mbalimbali.

Pia wanawake kupatiwa elimu ya ujasiriamali, kutambua haki zao pamoja na lishe kwa watoto ukizingatiwa kwamba mkoa huo una changamoto ya kuwepo kwa udumavu wa watoto kwa asilimia 56.9

No comments