Breaking News

Rais Magufuli aruhusu Waislamu kuendelea kujenga msikiti.


Na Mussa Mwangoka, Rukwa.

Rais Dk. John Magufuli amemaliza mgogoro wa ujenzi wa nyumba ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu iliyopo katika eneo la bomani mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Rais Magufuli amechukua uamuzi huo ikiwa ni siku chache tangu waumini wa dini ya kiislamu kujitokeza hadharani kupinga uamuzi wa mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo kushinikiza uongozi wa halmashauri ya Manispaa kuzuia ujenzi huo.
Akizungumza mapema leo Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alisema Rais Magufuli amemwagiza awaruhusu viongozi wa jumuiya ya  Istiqaama Sumbawanga, kuendelea na ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada.

Alisema kwamba aliwasiliana na Rais Magufuli jana kwa njia ya simu ambapo alitoa maagizo kwamba waendelee na ujenzi wa msikiti huo ambapo kibali kutoka wizarani cha kubadili eneo hilo kutoka eneo la makazi kuwa nyumba ya ibada kitafuata.

Mkuu huyo wa mkoa alisema alilazimika kuzuia ujenzi huo usiendelee kwa kuwa alibaini kuna baadhi ya taratibu ikiwa ni pamoja na kutokuwa na kibali kutoka wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi zilikiuka hivyo alitaka taratibu hizo zifuatwe ndio ujenzi huo uendelee.

Aidha, baadhi ya wenyeviti wa serikali ya mtaa wa bomani walimfuata mkuu huyo wa mkoa na kumlalamikia juu ya ujenzi wa msikiti huo katika eneo la makazi ya watu pasipo kufuata taratibu za matumizi ya ardhi hiyo.

Baada ya zuio hilo waumini wa dini ya kiislamu wakiongozwa na Shekhe wa mkoa huo, Rashid Akilimali walipanga kufanya maandamano makubwa ya amani siku ya alhamis ikiwa ni kushinikiza zuio hilo liondolewe mara moja.

Shekhe huyo alinukuliwa akisema pamoja na kufanya maandamano hayo, pia wamekubaliana kususia shughuli zote za kiserikali ambazo mkuu wa mkoa huo, Joachim Wangabo atashiriki wakidai yeye ndiye alishinikiza kuzuia msikiti huo usiendelee kujengwa kwa madai ya kutofuatwa kwa taratibu.

Alienda mbali zaidi na kudai wao hawana imani na kiongozi huyo wa mkoa wa Rukwa,kwa kuwa yeye ndiye aliyeshinikiza kutolewa kwa zuio hilo la ujenzi wa msikiti wakati wakuu wengine wa mikoa waliopita wakujishughulisha na ujenzi wa msikiti huo.

Mgogoro wa ujenzi wa msikiti huo umedumu kwa zaidi ya miaka saba sasa ambapo mara kadhaa uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga umekuwa ukizuia ujenzi wake kwa kutoa hati ya zuio lakini viongozi wa jumuiya hiyo wamekuwa wakipuuza na kuendelea na ujenzi.

Mgogoro baina ya viongozi wa jumuiya Istqaama Sumbawanga na wakazi wa eneo hilo kuhusu ujenzi wa msikiti huo umeanza tangu mwaka 2010, ambapo wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi ndio imekuwa ikisuasua kutoa kibali hicho hadi sasa.

Mwenyekiti wa jumuiya ya Istiqaama Sumbawanga, Seif Mohamed Aljabri alimshukuru rais kwa maamuzi yenye hekima na busara ambayo yamemaliza mgogoro huo, uliodumu kwa muda mrefu sana.

Alisema uzembe wa baadhi ya watendaji wa serikali ndio ulifanya mgogoro huo kufikia hatua hiyo, kwa kuwa wao walikuwa na haki zote za kuendelea na ujenzi kwani walifuata taratibu na waliochelewesha kibali ni wizara husika.

No comments