Breaking News

Kijana aenda jela miaka 23 kwa hatia ya wizi

Mwandishi wetu 
Katavi.

Mahakama ya Wilaya Mlele mkoani Katavi imemuhukumu  Omary  Ally (20)  kifungo  cha  miaka   23 jela  baada ya kupatikana  na  kosa  la   kuvunja na  kuiba  nyumbani kwa  Ofisa  mipango  wa  Halmashauri ya  Wilaya ya  Mlele.

Hukumu hiyo ilitolewa jana  na  Hakimu  Mkazi wa  Mahakama ya Wilaya ya  Mlele, Teothimu  Swai baada ya  mshitakiwa kukili makosa  mawili aliyosomewa mahakamani  hapo ya kuvunja na kuiba.

 Awali  katika  kesi  hiyo, mwendesha  mashitaka  mkaguzi wa Polisi, Baraka  Hongela  alidai  mahakamani  hapo kuwa mtuhumiwa  alitenda kosa  hilo machi  29  mwaka huu nyakati za saa tisa usiku nyumbani kwa ofisa wa serikali.

Inadaiwa kwamba, siku  hiyo  ya  tukio  mtuhumiwa alivunja  nyumba ya  afisa  mipango wa Halmashauri ya  Wilaya ya Mlele  Afred  Sungura,kisha aliiba Laptop moja.

Mshitakiwa  huyo  baada ya kusomewa  mashitaka  hayo  mawili alikiri  Mahakamani  hapo  kutenda  makosa  hayo kwa makusudi, kwa madai alipitiwa na shetani tu ndio maana akalazimika kufanya wizi huo.

Hakimu  Mkazi  Swai alimhoji mshitakiwa huyo iwapo ana sababu ya yoyote ya kujitetea ili kuishawishi mahakama impunguzie adhabu.

Katika  utetezi  wake mshitakiwa,  aliomba  mahakama impunguzie  adhabu  kwa kuwa  bado ana umri   mdogo wa miaka (20)  maombi hayo ambayo yalipingwa  vikali na  mwendesha  mashitaka, Hongela na kuiamba  mahakama  itoe   adhabu  kali kwa mshitakiwa ili kukomesha watu wengine  wenye  tabia  kama  hiyo.

Hakimu Swai baada ya kusikia tetezi  huo alimhukumu mshitakiwa huyo kwenda kutumikia kifungo cha miaka 23 jela ili iwe fundisho kwa watu wengine.

No comments