Breaking News

AMANI KUTOWEKA NCHINI KWA KUWA WATAWALA WAMEKOSA HOFU YA MUNGU , ASEMA ASKOFU.

 Wachungaji wa umoja wa makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT)katika manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa wakiendesha ibada maalumu ya kuliombea amani taifa baada ya kutimiza miaka 50 tangu kupata uhuru.

VIONGOZI umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania-CCT mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, wametabiri kwamba uenda amani iliyopo sasa ikatoweka kabla taifa hili halijatimiza miaka 100 tangu kupata uhuru kutokana na watawala wa sasa kukosa hofu ya mungu.

Askofu wa Kanisa la Anglikana, Maiko Baledeya alisema hayo jana wakati wa ibada maalumu ya kuliombea amani taifa hili baada ya kutimiza miaka 50 tangu kupata uhuru, ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lililopo mjini hapa.

Askofu Badeleya alisema kuwa watawala wanapokosa hofu ya mungu maana yake wanakuwa si wazalendo kwa taifa lao hali ambayo imechangia kuongezeko la mmomonyoko wa maadili, huku rushwa na ufisadi vikitawala pasipo kudhibitiwa.

"watawala wetu hawana hofu ya mungu ndio maana ya wamekosa uzalendo.....ni tofauti kabisa kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere ambaye kwanza alikuwa ni mcha mungu hivyo akawa na hofu ya mungu na uzalendo wa hali ya juu" alisema Askofu huyo.

Aliongeza kuwa hali ikiendelea kuwa hivi ilivyo taifa halina miaka mingine 50 ya amani na utulivu kama ilivyo sasa kutokana kuwapo kwa kizazi chenye mchanganyiko huku kikikosa maadili, kutomuogopa mungu na kukosa uzalendo, kutokana na baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali kutowajibishwa kwa kashfa mbalimbali walizonazo ikiwamo ya ufisadi.

Askofu huyo aliwataka wazazi kuwalea watoto wao katika misingi ya kumuogopa  na kumuheshimu mungu ili taifa lipate watu wenye maadili na wazalendo wenye kulinda na kutetea rasilimali za nchi yao.

Katika ibada hiyo, viongozi wa CCT Sumbawanga mjini, walitoa tamko katika kuadhimisha miaka 50 ya uhuru ambapo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mchungaji Israel Moshi , alisema kuwa tamko hilo limeelekeza kutaja mambo ambayo ni hatari kwa ustawi wa taifa letu.

Baadhi ya mambo hayo ni ufisadi na rushwa ambayo kwa sasa ni janga la taifa ambapo kama hakuna mpango mahususi wa kupambana nayo basi maadhimisho ya miaka 50 hayatakuwa na maana kwa watanzania.

Aliongeza kuwa ukiukwaji wa katiba na utawala wa sheria unajenga hisia za kuondoa usawa miongoni mwa watanzania hasa pale unapogusa matabaka ya kidini na viongozi.

Mchungaji huyo aliitaka Serikali kuondoa tabaka na nafasi inayoendelea kujengwa baina ya walionacho na wasio nacho, watawala na watawaliwa ni jambo hatari sana lishughulikiwe mara moja ili kujenga taifa lenye usawa.


Waumini wa makanisa ya umoja wa Kikristo Tanzania (CCT) manispaa ya Sumbawanga wakiimba wimbo wa taifa wakati ibada hiyo.

No comments