Breaking News

AMTWANGA RISASI NA KUMJERUHI NDUGU YAKE MKESHA WA MWAKA MPYA.

KIJANA Onesmo Kaniki (37) mkazi wa kijiji cha Senga -Kilonge wilayani Sumbawanga amenusurika kufa baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa  vibaya siku ya mkesha wa sherehe za mwaka mpya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa,Isuto Mantage tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari Mosi mwaka huu, alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Nestory Kaniki (20) mkazi wa kijiji hicho cha Senga -Kilonge ambaye ni mdogo wake Onesmo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa mjini Sumbawanga .

Onesmo amelazwa hospitalini hapo,wodi namba tatu akiwa amejeruhiwa vibaya na risasi, chini ya ziwa lake la upande wa kushoto ambapo hali yake imeelezwa kuwa sio nzuri.

Akielezea mkasa huo, Fanueli Kaniki ambaye ni kaka yao mkubwa na majeruhi huyo, na ndiye anayemuuguza katika hospitali hiyo alisema kuwa hali ya mgonjwa si nzuri sana lakini anaendelea kupata matibabu.

Alisema kuwa chanzo cha mkasa huo ni kwamba usiku huo wa mkesha wa mwaka mpya ndugu hao wawili na kundi la vijana wenzao walikusanyika mashambani karibu na kijiji hicho katika kibanda cha John Myemba, wakinywa pombe ya kienyeji 'ndelike'.

Ndelike kwa mujibu wa Fanueli ni pombe inayonywea bure wakati wa sherehe hivyo John alitengeneza pombe hiyo na kuwaalika vijana hao kujumuika nae katika kusheherekea Mkesha wa Mwaka Mpya.

Alisema mara baada ya vijana hao kunywa na kuanza kuchangamka walianza kucheza ngoma ya kienyeji, ndipo Onesmo alimdhihaki mdogo wake Nestory kuwa hajui kucheza kauli iliyomghadhabisha.

'Nestory alikasirishwa na kauli hiyo ya dhihaka ya kaka yake aliyodai iliyojaa dhihaka na kejeli ambapo aliapa kumpa somo la mwaka mpya kaka yake huyo ndipo alipomvizia njiani akiwa na bunduki aina ya gobole aliyokuwa ameishindilia baruti ambapo kaka yake alipomkaribia alimfyatulia risasi iliyomjeruhi kaka yake huyo.

Baada ya kutenda unyama huyo mdogo wake alikimbia akiamini kuwa amemuua kaka yake na anasakwa na polisi mkoa wa Rukwa.

No comments