Breaking News

POLISI WAUA MTUHUMIWA KWA RISASI AKIWA CHINI YA ULINZI.

KIJANA Osward January (30) Mkazi wa kitongoji cha Lyazumbi, kijiji Paramawe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, amefariki dunia baada ya kupingwa risasi wakati akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kijana huyo alifariki nyakati za saa 6 mchana januari 2 mwaka huu wakati akiwa hospitali teule ya wilaya ya Nkasi iliyopo mjini Namanyere ambako alipelekwa kwaajili ya kupata matibabu kutokana kupata majeraha ya risasi alizopingwa.

Inadaiwa kijana huyo alipingwa risasi hizo na askari aitwaye PC Molton Magesa, aliyekuwa ameambatana na askari wenzake saba ambao walikuwa wamebeba silaha aina ya SMG na risasi za moto, ambapo alipingwa risasi hizo sehemu ya ubavu wa kulia na kutokea upande wa kushoto.

Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, chanzo cha kijana huyo kupigwa risasi ni kutokana na purukushani baina yake na askari hao baada ya kukamatwa kwa tuhuma ya kuhusika kuvunja nyumba anayoishi mhandisi Suleiman Athuman (41) katika kambi ya wachina wa kampuni ya kichina ya iitwayo CHCEG ambayo inajenga barabara  kutoka Kanazi - Kizi - Kibaoni kwa kiwango cha lami.

Inasemekana kuwa wakati askari hao wakiwa katika harakati za kumkamata mtuhumiwa huyo, aliwatishia kuchoma kisu na kuwakata na mapanga ambapo askari hao walijipanga na kufanikiwa kumkamata kijana huyo, lakini akiwa chini ya ulinzi wa polisi alirusha kisu alichokuwa akimlenga polisi mmojawapo.

Lakini kisu hicho kilimkosa na kutoboa koti kisha kumkwaruza sehemu za kwapa kuona polisi huyo, hivyo Pc Molton alifyatua risasi kwa lengo la kumpiga miguuni lakini ikampata ubavuni na baadaye kufariki dunia.

Kamanda huyo alisema kuwa baada ya kijana huyo kupingwa risasi na kutokea upande wa pili, ilimkuta Chacha Machage (34) mkazi wa kabwe aliyekuwa akipita jirani na eneo hilo ambaye alijeruhiwa sehemu ya mkono wa kulia ambaye naye alipelekwa hospitalini na kuruhusiwa baadaye baada ya kupata matibabu.

Aidha, inaelezwa kuwa awali katika nyumba ya Mhandisi huyo, kijana huyo na mwenzake aitwaye Gallus Sambi waliiba Tv, magodoro mawili, deck moja na micro wave na vitu vingine ambavyo thamani yake haijajulikana ambapo msako wa kuwasaka watu hao kwa ushirikiano wa polisi, walinzi wa kampuni hiyo na wananchi ulianza mara moja.

Inaelezwa kwamba  januari 2 alfajiri wananchi walibaini kwamba vitu hivyo vimefichwa nyumbani vijana hao ambao walikuwa wakijihami kwa visu na mapanga ambapo mwisho wa siku kijana Sambi alikimbia na kumuacha mwenzake akipatwa na dhahama hiyo.

Kamanda Mantage, alisema kuwa kijana huyo anaendelea kutafutwa huku Askari Pc Molton anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi ili kubaini kama  ana hatia ili sheria ichukue mkoando wake.

No comments