WATU wasiojulikana wanadaiwa kuvamia katika Shule ya Sekondari ya Lusaka iliyopo kata ya Lusaka wilayani Sumbawanga na kufanya uharibifu mkubwa wa majengo na kuiba vitu mbalimbali vilivokuwa kwenye stoo ya shule hiyo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Crispin Luanda uvamizi na uhalibifu huo ulifanyika Usiku wa kuamkia Desemba 27 mwaka jana.
Kufuatia taarifa za uhalifu huo timu ya wataalamu kutoka ofisi ya mkurugenzi ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo , Luanda ilitembelea shule hiyo na kushuhudia uharibifu mkubwa uliofanywa na wavamizi hao, ambapo suala hilo linafanyiwa kazi na halmashauri kwa kushirikiana na vyombo vya usalama.
Kwa mujibu wa Luanda , tathimini ya awali iliyofanyika imebaini kuwa hasara iliyopatikana kutokana na uhalibifu wa majengo wa shule hiyo ni Sh 2,570,000.
“Uharibifu uliofanywa ni kuvunjwa kwa vioo vya madirisha katika ofisi ya Mkuu wa shule pamoja na kuvunjwa kwa vioo vya madirisha katika nyumba mbili za walimu ikiwemo ya mkuu wa shule.
Wahalifu hao pia walivunja stoo ya shule na kuiba mahindi kiasi cha gunia moja na debe tatu yaliyokuwa yakitumiwa na wanafunzi wa shule hiyo’ alisema Luanda
Kaimu Mkurugenzi huo alitanabaisha kuwa wakati wa tukio hilo linalodhaniwa kufanywa saa nane za usiku,walimu walikuwa ndani wamelala na baada ya kugundua kuwa wamevamiwa walianza kuwasiliana kwa simu za mkononi na kupeana taarifa kabla ya wavamizi hao kutokomea kusikojulikana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa , Isuto Mantage hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo kwamba uchunguzi na msako wa kuwabaini wahalifu hao unaendelea ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Shule hiyo ya Lusaka imekuwa ikikumbwa na mikasa ya mara kwa mara ambapo Machi 19 mwaka jana Serikali iliamua kuifunga shule hiyo kwa muda usiojulikana baada ya wanafunzi kutaka kuwaua walimu wao kwa kuwachoma na moto wakiwa wamelala. |
No comments