Breaking News

UADILIFU WA VIONGOZI NDIO MUAROBAINI WA KUTIBU SHIDA ZA WANANCHI LAKINI SI KATIBA MPYA PEKEE.

Mbunge wa jimbo la Kalambo, Josephat Kadege akizungumza na wananchi wa jimboni kwake hii leo wakati akifungua mdahalo wa kuhamashisha wananchi wengi kushiriki katika mchakato wa kupata katiba mpya.

KATIBA mpya ijayo haitakuwa muarobani wa kutibu shida zote za wananchi kama viongozi hawatakuwa waadilifu na wazalendo kwa Taifa lao.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mbunge wa Jimbo la Kalambo Wilayani Sumbawanga,Josephat Kandege wakati akifungua mdahalo wa kuhamasisha wananchi wengi kushiriki katika mchakato wa kupata katiba mpya.

Mdahalo huo ulioandaliwa na muungano wa asasi zisizo za kiserikali (RANGO) mkoani Rukwa  unaofadhiliwa na The Foundation for Civil Society na kufanyika katika Tarafa ya Matai, Jimbo la Kalambo wilayani humo.

Alisema kuwa Watanzania  kamwe wasitegemee kupata maendeleo endelevu kwa kupitia Katiba Mpya iwapo viongozi hatakuwa waadifu na wananchi wasipokuwa wazalendo.

'Viongozi na wananchi kwa pamoja wanatakiwa kuwa waadilifu,wazalendo na watangulize maslahi ya  taifa kwanza kama kweli wanataka kuona maendeleo ya kweli na ndipo hapo tutakapoona faida ya Katiba Mpya tunayoisubiri kwa hamu' alisema.

Pia aliwahimiza wananchi wa Jimbo la Kalambo kujitokeza kwa wingi mara baada ya tume ya kukusanya maoni juu ya katiba mpya itakapoanza kufanya kazi ili waweze kushiriki ipasavyo katika mchakato huo na si kalalamika pasipo kuonyesha ushiriki wao.

Alisema kujitoa na kutoshiriki katika utoaji wa maoni ni kujisaliti wenyewe kwa kuwa kunaweza kusababisha kuundwa kwa katiba isiyoweza kutatua kwa asilimia kubwa changamoto zilizopo kwenye maeneo yao.

 Alilalamikia upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa kuwa katiba hii ya sasa haifai kwamba kupitia katiba hii wanayoibeza ndiyo chimbuko la kutukuka kwa nchi hii.

Alisisitiza kuwa midahalo kama hiyo kufanyika kwa wingi ili wananchi waweze kujiandaa ipasavyo na kutoa maoni yenye kuleta katiba itakayomjali kila mmoja na kumlinda.

Aidha  aliwataka wananchi kutambua kuwa majadiliano juu ya katiba yanapaswa kulenga maslahi ya taifa na si chama chochote cha siasa.

Katibu Mtendaji wa RANGO,Stanley Mshana alisema upo umuhimu mkubwa wa makundi mbalimbali wakiwemo wazee,walemavu, wanawake, vijana kushiriki kikamilifu katika mchakacho wa kupata Katiba Mpya.
 
Mkazi wa tarafa ya Matai katika jimbo la Kalambo wilayani Sumbawanga, Agustino Machenguli, akichangia mada katika mdahalo huo leo asubuhi.
Baadhi ya wananchi wakiwa katika picha ya pamoja na Mbunge wa jimbo la Kalambo, Josephat Kandege leo asubuhi wakati wa mdahalo wa kuhamashisha wananchi wengi kushiriki katika mchakato wa kupata katiba mpya.

No comments