Breaking News

WANAKIJIJI RUKWA, WAMKATAA MWENZAO MBELE YA MKUU WA MKOA

Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Milepa kilichopo wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa kijiji hicho wamrejeshe mkazi mwenzao ambaye walimfukuza kwa madai ya unyanyasaji na kuwalipisha faini wenzake kinyume na taratibu, kwa  habari zaidi soma hapo chini.
WANANCHI wa kijiji cha Milepa kilichopo wilayani Sumbawanga,  jana wamemfukuza rasmi mbele ya uongozi wa mkoa wa Rukwa, mkazi mwenzao anayedaiwa kuwa kinara wa vitendo vya unyanyasaji na kuwalipisha faini wananchi wenzake kinyume na utaratibu.

Mkazi huyo aitwaye Said Mohamed (40) ambaye awali walitangaza kumtimua kijiji hapo mei 30 mwaka jana, alipeleka malalamiko yake ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa, ambapo jana mkuu huyo wa mkoa, Stella Manyanya, akiwa na viongozi wengine wa mkoa na wilaya walilazimika kufika kijiji hapo kwa lengo la kusaka suluhu lakini wananchi hao walikataa kumpokea mkazi huyo.


Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika uliofanyika kijiji hapo jana, baadhi ya wananchi waliopewa fursa hiyo walisema kuwa hawako tayari kuishi katika kijiji hicho na Mohamedi kwa kuwa amewafanyia vitendo vya uonevu na unyanyasaji kwa muda sasa.


Vitendo hivyo ni pamoja na kuwalipisha faini kubwa kunyume na utaratibu wakati pia yeye si kiongozi wa kijiji, ambapo mara kadhaa mifugo inapoingia katika shamba lake au kupita nyumbani kwake amekuwa akitoza faini kuanzia shilingi 300,000 hadi 500,000 kitu ambacho kinawaumiza wananchi na wale wasio na uwezo wa kulipa faini hizo amekuwa akikamata mifugo yao na kuichinja.


Mmoja wa wananchi hao, Potino Simfukwe alisema kuwa kamwe hawawezi kumruhusu Mohamedi kuendelea kuishi kijijini hapo, kwa kuwa wamechoka vitendo vyao vya dhuruma na uonevu ambao ameufanya kwa muda mrefu sasa.


"hatuwezi kumpokea huyo mtu...... mkuu wa mkoa tunakuheshimu sana tunaomba ondoka naye kwa kuwa tofauti na hivyo ipo siku polisi watakuja na kukamata watu wote hapa kijijini na kupeleka jela" alisema Simfukwe pasipo kufafanua.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho, Godfrey Njelu aliongeza kuwa malalamiko dhidi ya Mohamedi ya muda mrefu sasa na kijiji kilishafanya uamuzi wa kumfukuza katika mkutano wa hadhara wa kijiji ambao mihustari yake ipo hivyo wao kama viongozi wanatekeleza maagizo ya wananchi na si vinginevyo.


Akijibu hoja hizo Mohamedi ambaye ni mzaliwa katika kijiji hicho, alisema kuwa chanzo cha viongozi hao kumchukia na kushinikiza wananchi wamfukuze ni kwa sababu amekuwa akitumia fursa ya uelewa alionao.


Kuhoji baadhi ya mambo yanavyoendeshwa hapo kijijini hapo ambapo mara kadhaa amehoji katika mikutano ya hadhara kwamba vifaa vya ujenzi

katika miradi ya jamii (Tasaf) vilivyokuwa vimebaki mahali vilikopelekwa.

Pia alihoji uingiaji wa wafugaji wa ng'ombe wakiwa na makundi makubwa ya mifugo pasipo kufuata taratibu wakati kijiji hakina maeneo ya malisho, upasua mbao kiholela pasipo vibali, Uvuvi Haramu, mapato na matumizi ya kijiji kwani ni mwaka wa pili tangu aanze kuhoji hakuna majibu yanayoridhisha.


Kwa upande wake Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa hali ilipofikia ni mbaya na hawezi kupinga uamuzi wa wanakijiji hao ila kinachoweza kufanyika kwa sasa ni mwananchi huyo kukaa na kutafakari ni namna gani atakavyoendesha maisha yake eneo jingine,kwa amani na utulivu huku uongozi wa mkoa ukiangalia ni hatua zipi utachukua ili kuweza kumsaidia mkazi huyo na familia yake lakini kwa sasa inabidi arejee mjini Sumbawanga kwa muda akisubiri taratibu hizo kufanyika.

No comments