Breaking News

RANGO WAENDELEA NA MIDAHALO YA KUELIMISHA WANANCHI RUKWA.

 Katibu Mtendaji wa Rango, Stanley Mshana, akitoa mada katika mdahalo juu ya ahadi za viongozi na utekelezaji wake uliofanyika katika tarafa ya Mpui jana. habari zaidi soma hapo chini.

IMEELEZWA kuwa kutoelimishwa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kumiliki ardhi,rushwa na urasimu wa baadhi ya watendaji wa serikali za mitaa ni miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la migogoro ya ardhi baina ya wananchi na wawekezaji.

Mjumbe wa bodi ya Muungano wa taasisi zisizo za kiserikali mkoani Rukwa (Rango) na mratibu wa masuala ya elimu wa haki za binadamu wilaya ya Mpanda, Suleiman Tumaini, alisema hayo kwa nyakati tofsauti wakati akitoa mada katika Mdahalo wa ahadi za viongozi na utekelezaji uliofadhiliwa na Shirika la The foundation for Civil Society na kufanyika katika za tarafa ya Mpui na Kasanga wilayani Sumbawanga.

Alisema kuwa watendaji wengi wa Serikali hasa katika ngazi za wilaya, kata na vijiji wamekuwa na urasimu katika utoaji wa maelekezo kwa wananchi namna ya kupata hatimiliki ya ardhi ya kimila, ambapo matokeo yake ni wananchi wengi wamejikuta wakiporwa maeneo yao na wawekezaji na kusababisha migogoro ya ardhi isiyokwisha.

"kupata hatimiliki ya ardhi ya kimila sio kazi ngumu lakini urasimu uliopo kwa watendaji wa Serikali na kuweka mbele rushwa ndio umesababisha wananchi kukosa haki ya kumiliki maeneo yao na matokeo yake ni migogoro baina ya wawekezaji, Serikali za vijiji na Serikali kuu ......... sasa badilikeni muwabane viongozi wenu mliowachagua wahakikishe mnapata elimu ....itawasaidia na migogoro nayo itapungua" alisema Tumaini.

Aliongeza kuwa faida ya kuwa na hatimiliki ya ardhi ni kuweza kupata mikopo hivyo kuweza kukopesheka katika taasisi za kifedha zikiwamo benki hali ambayo itasaidia kukuza mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara hivyo kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Tumaini alisema kuwa pia ni wajibu wa viongozi tuliowachagua kuonyesha mikakati ya kushughulikia kwa wakati migogoro ya ardhi, ili haki iweze kutendeka kwani uzoefu unaonyesha kwamba viongozi hao wamekuwa hawataki kujihusisha katika mipango ya kumaliza migogoro hiyo hivyo imefikia hatua ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na mali pia kuongezeka kwa chuki na uhasama miongoni mwa raia.

Alisema kuwa ni vema viongozi hao waeleze mikakati ya kukuza uelewa wa wananchi juu ya masuala ya ardhi, jinsi ya kupigania na kuondolewa kwa mianya iliyopo katika sheria ya ardhi yenye kuzaa mazingira kandamizi, mathalani sheria namba 4 katika sheria ya ardhi ya mwaka 1999.

Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa baadhi ya mikoa nchini ambayo wananchi wake wamekuwa na migogoro mingi ya ardhi kutokana na kufuatwa kwa sheria ya ardhi pindi wapopatiwa maeneo kwaajili shughuli za kilimo, ufugaji na uwekezaji.


Baadhi ya wananchi wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa katika mdahalo wa ahadi za viongozi na utekelezaji wake, juzi katika kijiji cha Kasanga.
Mwl. Josepha Michese akitoa mada katika mdahalo wa ahadi za viongozi na utekelezaji wake, juzi katika kijiji cha Kasanga jimbo la Kalambo.

No comments