Breaking News

Elimu ya afya ya uzazi yatajwa ndio mwarobaini wa mfumo dume Rukwa

ELIMU ya afya ya uzazi ambayo wanaume wa vijiji vya tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamekuwa wakinufaika nayo imetajwa ni chachu ya kuimarisha ndoa zao na kupunguza visa vya ukatili na unyanyasaji  wa kijinsia  unaotokana  na mfumo dume.
 Baadhi ya wakazi wa vijiji vilivyopo tarafa ya Mtowisa wakiwa wamewapeleka watoto wao kliniki kama walivyokutwa na mpiga picha wetu jana katika kituo cha afya Mtowisa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na waandishi wa habari kwenye kituo cha afya Mtowisa, baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo walikiri kuwa yote yamewezekana  kutokana na  hamasa  kubwa iliyofanywa na mradi  wa Wazazi na Mwana kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi.

Ambayo inayokwenda sambamba na kuhamasisha ushiriki wa wanaume katika  katika masuala ya uzazi kwa kumsindikiza mkewe kliniki kabla na baada ya kujifungua ukilenga kufikia malengo ya kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 75 ifikapo 2015.

"Hakuna  tena  kitu kinachoitwa  mfumo  dume kwetu  kwani sasa  mume wangu  ananisindikiza kliniki  kila mara  ili kupata ushauri  wa kitaalamu  hususani ninapokuwa  mjamzito  pia  ananisaidia kazi  mbalimbali  za  nyumbani.......vipigo vimepungua kama sio kwisha kabisa, kimsingi elimu imesaidia sana" alisema Beatrice Milambo.
Afisa muuguzi wa uzazi salama katika hospitali ya mkoa wa Rukwa, Fides Nduasinde akitoa mada katika mafunzo utepe mweupe ya wajibika mama aishi kwa wakina mama wajawazito wa vijiji vya tarafa ya Mtowisa.

Naye, Chrispin Mponje alisema kwamba mwamko kuhusu wanawake kujifungulia katika vituo vinavyotoa huduma ya afya ni mkubwa hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kwenye maeneo hayo tofauti na ilivyokuwa awali.

Kwa upande wake, Kaimu mganga mkuu wa kituo cha afya Mtowisa, Dk Raphaeli Kyando alisema kuwa baada ya mradi huo kuanza kutoa elimu takribani miaka miwili iliyopita kuna mabadiliko makubwa sana kwani katika kipindi cha mwezi mmoja wanawake zaidi kati 75 hadi 100 wanajitokeza kujifungulia kwenye zahanati na vituo vya afya tofauti na awali ni idadi yao ilikuwa kati ya 20 hadi 35 kwa mwezi.
 Wenzi wakipata maelezo kutoka mtaalamu wa afya baada ya kuhudhuria kliniki ya baba na mwana jana katika kituo cha afya Mtowisa.

Aliongeza kuwa pamoja na elimu hiyo wanayopata lakini kituo hicho cha afya kimeweka utaratibu kwamba kila mwanamke anayekwenda kufungua kadi ya kliniki ili aanze kupata huduma baada kupata ujauzito ni lazima aende na mume wake tofauti na hivyo hawezi kupokelewa hali ambayo imefanya wanaume wengi wajitokeze na kupatiwa elimu ya afya ya uzazi na viashiria vya hatari kabla ya mama mjamzito kujifungua.

Mratibu wa mradi wa Wazazi na Mwana wilaya ya Sumbawanga, Gasper Materu alisema kuwa elimu ya afya ya uzazi imekuwa mtambuka ambapo kwa sehemu kubwa imesaidia kupunguza kwa mauaji ya kujichukulia sheria mkononi yaliyokuwa yakihusisha wanandoa mkoani Rukwa kwa kuwa hivi sasa  wanandoa wamekuwa wakishirikiana katika kutoa maamuzi ya kifamilia tofauti na ilivyokuwa awali.

No comments