Breaking News

Wakulima waitaka Serikali kununua tani zaidi za mahindi

WAKULIMA mkoani Rukwa imeitaka Serikali kupitia kitengo cha mamlaka ya taifa ya uhifadhi wa Chakula (NFRA) kuongeza tani za ununuzi wa mazao ya mahindi ili wakulima wengi waweze kunufaika na soko hilo la mazao hayo.
    Mahindi yakiwa nje ya kituo ununuzi cha Mtowisa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa jana walipofikishwa na wafanyabiashara baada NFRA kuanza ununuzi wa mazao hayo ambapo gunia moja wananunua kwa bei ya Sh 50,000

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti jana kwenye kijiji cha Mtowisa wilayani Sumbawanga ambako kuna kituo cha ununuzi wa mazao hayo walisema kuwa tani ambazo NFRA imepanga kununua msimu huu ni kidogo ukilinganisha na mazao yaliyozalisha.

"mathalani katika ukanda huu wa bonde la ziwa Rukwa, tumezalisha mahindi mengi sana msimu huu.....hivyo serikali kununua tani 40,000 pekee ni chache ukilinganisha na mavuno tuliyopata hivyo....binafsi niiombe serikali iongeze idadi ya tani ambazo itanunua" alisema Didas Malingumu.

Naye Diwani wa kata ya Muze, Kalolo Ntila alisema kuwa iwapo Serikali itaongeza idadi ya tani ambazo itanunua ni wazi kwamba wakulima wengi watanufaika na soko hilo ambalo kimsingi lina tija kwao kwa kuwa NFRA inanunua kilo moja ya mahindi Sh 500 sawa na gunia moja kwa Sh 50,000 bei ambayo inampa manufaa mkulima.

Aliongeza kwamba bei hiyo ambayo NFRA wananunua mahindi kwa sasa nzuri na mkulima hawezi kuipata kwa wafanyabiashara wengine kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakinunua gunia moja kwa bei ya kati Sh 25,000 hadi 30,000 hali ambayo ni kumdidimiza mkulima.

Diwani Ntila alisema kuwa mathalani kituo hicho cha Mtowisa kimepangiwa kununua  tani 1800 na kwa kuanzia kinanunua tani 700 pekee ambazo ni kidogo ukilinganisha na mwamko wa wakulima kujitokeza kwa wingi na kufikisha mahindi yao kwa ajili ya kufanya biashara hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa NFRA mkoa wa Rukwa, Amos Mtafya alisema kuwa wanachokifanya sasa ni kutekeleza mpango wa Serikali ambayo ni kununua tani 40,000 kwa msimu huu katika mikoa ya miwili ya Rukwa na Katavi.

Alisema kwamba NFRA kununua tani kidogo msimu huu ukilinganisha na ule uliopita ambapo mamlaka hiyo ilinunua tani 50,117.113 katika mikoa hiyo miwili, sehemu tu ya mpango wa Serikali  na fursa kwa wafanyabiashara wengine pia kujitokeza kununua mazao hayo.

Mkoa wa Rukwa pekee unatajwa kuwa na ziada ya tani za mahindi zaidi 360,000 hali ambayo inafanya ununuzi huo kuwa ni kiduchu sana ukilinganisha na uzalishaji uliofanyika katika msimu wa kilimo uliopita.

No comments