Kukimbilia kwa waganga wa kienyeji sio suluhu la matatizo ya uzazi
WANAWAKE wametakiwa kuacha dhana iliyojengeka miongoni mwao
kuwa waganga wa jadi ndio suluhu la kutibu maradhi ya kukosa watoto
badala yake waende na wanaume zao kwenye Kliniki za afya ili wapate
uchunguzi zaidi wa kitabibu na kutatua tatizo hilo.
Mratibu mradi wa shirika la Swedish Association for
Sexuality Education (RFSU) Dk. Cuthbert Mendaenda,alisema hayo wakati
akitoa mada kwenye mafunzo ya afya ya uzazi na ujinsia kupitia mradi wa
Tanzanian Men as Equal Partners (TMEP)yaliyoshirikisha waandishi wa
habari kutoka mikoa ya Singida na Rukwa ambayo yanafanyika katika ukumbi
wa Kalenga west Park Hotel uliopo mjini hapa.
Dk. Maendaenda alisema kwamba zipo sababu nyingi
zinazochangia wanaume na wanawake kukosa watoto likiwemo suala la
mzunguko wa hedhi kwa wanawake hivyo sasa iwapo wote hawafahamu kuhusu
jambo hilo ni vugumu kupata suluhu ya tatizo hata wakienda kwa waganga
wa kienyeji.
Pia aliongeza kwamba jamii
inapaswa kuondokana na dhana potofu kuwa mwanaume wakifunga uzazi
wanapoteza uwezo wa kufanya tendo la ndoa kabisa kitu ambacho
kinasababisha wanaume wengi kutokubali kufunga uzazi hivyo kuzaa watoto
wengi bila kufuata uzazi wa mpango.
"Tusaidie kuelimisha na jambo hili, wanaume hawataki
kufunga uzazi kwa kisingizio cha kupoteza nguvu za kiume.....si kweli ni
taarifa ambazo zimejaa upotoshaji mkubwa na hatupaswi kuufumbia macho"
alisema.
Kwa upande wake, Meneja mawasiliano wa RFSU, Eugenia
Msasanuri alisema kuwa mafunzo hayo kwa wanahabari wa mikoa ya Rukwa na
Singida yamelenga kusaidia kutoa elimu kwa jamii ya mikoa hiyo kuhusu
ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya afya ya uzazi hali ambayo
itapunguza mifumo dume ambayo imekuwa ikisababisha ndoa nyingi
kuvunjika.
Alisema kuwa jamii ikielimishwa na wanaume wakashiriki
kikamilifu katika afya ya uzazi itasaidia pia kupunguza vifo vya
wakinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hivyo malengo ya
Serikali kupunguza vifo hivyo kwa asilimia 75 ifikapo 2015 yanaweza
kufikiwa.
No comments