Breaking News

Watoto zaidi 9000 wapatwa na utapiamlo mkali mkoani Rukwa






WATOTO 9700 waliopo katika vijiji vya Kisumba, Kasote na Chisenga kwenye kata ya Kisumba vilivyoko wilayani Kalambo mkoani Rukwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la utapiamlo mkali kufuatia kuwepo kwa malezi duni kutoka kwa wazazi na walezi wao.


Hali hiyo imesababisha mkoa wa Rukwa kuwa miongoni mwa mikoa mitano ambayo inakabiliwa na tatizo la udumavu licha kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula hususani ni mahindi.

Baadhi ya wanawake wa kijiji hicho walisema hayo wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana wakati wa sherehe za siku ya afya kijiji iliyoandaliwa katika kijiji cha Kisumba iliyoandaliwa na shirika la Africare linalotekeleza mradi wa wazazi na mwana wenye lengo la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano mkoani humo.

Mmoja wa wanawake hao, Yusta Sangu alisema kuwa hali hiyo imejitokeza kutokana na kukosekana kwa elimu sahihi ya afya uzazi kwa muda mrefu kiasi cha kufanya wanawake wengi  wajifungulie majumbani bila kufuata uzazi wa mpango hivyo kuwa na idadi kubwa mno ya watoto




Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kisumba Kasanga, akitoa chanjo ya matone kwa mtoto mmoja wa mkazi wa kijiji hicho jana wakati wa siku ya afya kijijini hapo, iliyoandaliwa na  shirika la Africare linalotekeleza mradi wa Wazazi na Mwana unalenga kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto.

Kwa upande wake, Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kisumba, John Mwambebule alisema kukosekana kwa malezi bora kutoka wazazi na walezi ndio kumesababisha hali hiyo ambapo alitoa wito kwa wazazi na walezi hao kuacha mara moja utamaduni uliojenga wa kuwanyonyesha watoto kwa miezi miwili tu badala ya miezi sita kama inavyopaswa  na kisha kukimbilia kuwapa vyakula visivyofaa hivyo kusababisha kupata utapiamlo mkali na udumavu.

Naye, mratibu wa mradi wa wazazi na mwana wilaya ya Kalambo,Matrina Phedson kutoka shirika la Africare alisema kuwa wamelazimika kuwapa elimu ya afya ya uzazi imekuwa na wigo mpana ikiwemo suala la kuzingatia lishe bora kitu ambacho wameamua kukifanya kwa wakazi wa vijiji hivyo ili kunusuru tatizo la utapiamlo kwa watoto ambao umekuwa ukiwasababishia udumamavu
Kwa mujibu wa takwimu za sasa za Wizara ya  Afya  na Ustawi  wa Jamii mkoa wa Rukwa una nusu ya watoto wenye chini ya miaka mitano ni wadumavu kwa asilimia 50 kutokana na kukosa lishe  bora katika makuzi yao.
Mratibu wa mradi wa wazazi na mwana wilaya ya Kalambo,Matrina Phedson (katikati) kutoka shirika la Africare akitoa maelekezo kwa wahudumu wa afya vijiji kuhusu utengenezaji wa chakula chenye lishe bora kwa mtoto jana kwenye kijiji cha kisumba ya Kasanga wilayani Kalambo. Picha na Mussa Mwangoka

No comments