Madiwani Nkasi watimua kazi watendaji 18 kwa makosa mbalimbali
MADIWANI wa halmashauri ya wilaya Nkasi mkoani Rukwa
wamewatimua kazi watendaji 18 wa halmashauri hiyo na wengine wawili wakipunguziwa
mishahara baada ya kukutwa na makosa kadhaa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, Peter Mizinga akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
Kimulika Galikunga alisema jana kwamba madiwani wamefikia hatua ya kuwafukuza kazi
watumishi hao baada ya kuridhishwa na taarifa za tume mbalimbali zilizokuwa
zinawafuatilia watumishi hao na kufikia
hatua hiyo ya kuwafukuza kazi.
Alisema kuwa watumishi hao wamefukuzwa kwa makosa makubwa
mawili ambayo ni ya kukusanya fedha kwa wananchi na kuzitumia kinyume cha
utaratibu ikiwa ni pamoja na wengine kuwa watoro kazini kwa muda mrefu.
Alisema kuwa watumishi waliofukuzwa kuwa ni maofisa watendaji
wa vijiji 7 ambapo kati yao wawili wamepewa adhabu ya kupunguziwa
mshahara, pia wao wauguzi wa hospitali na Maafisa kilimo wasaidizi.
Mkurugenzi huyo alidai kuwa watumishi hao wamekumbwa na
tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma na wengine kwa utoro wa muda mrefu
kazini na baada ya uchunguzi wa kina makosa yao yamebainika na kuwa suluhisho
imekuwa ni kuwafukuza kazi watumishi hao.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi,
Kimulika Galikunga akisisitiza jambo katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo.
Pia katika kikao hicho, madiwani wa halmashauri hiyo
waliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kujipima sawasawa kama wana uwezo wa
kufanya kazi na kama hawana uwezo huo basi wawapishe kabla wao hawajachukua
hatua.
Akichangia katika kikao hicho mara baada ya kupata ripoti ya
mkaguzi mkuu mkazi na mdhibiti wa fedha za serikali mkoani Rukwa John Nalwanda
diwani wa kata ya Nkomolo Sospeter Kasawanga alidai kuwa ripoti ya mkaguzi huyo
ni nzuri na inaonyesha wao kupata hati safi katika kipindi cha mwaka 2012-13 na
kuwa hawataki tena kuona kuwa wanapata hati chafu au yenye mashaka.
Alisema ni muda mrefu sasa halmashauri hiyo imekua ikipata
hati zenye mashaka na kumpongeza mkurugenzi mtendaji wa sasa Kimulika Galikunga
kwa utendaji wake mzuri na kumtaka kuendelea
kuwasimamia watendaji wake hao ili waweze kufanya vizuri zaidi na kuwa
kwa kufanya hivyo wananchi ndiyo wanaonufaika kutokana na huduma za serikali
kuimarika.
Baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi wakifuatilia kwa makini kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo.
Diwani wa kata ya Kipili Kapunda Mbwilo aliwataka watendaji
hao kukaza uzi kutokana na taarifa nzuri ya mkaguzi na mdhibiti wa fedha za serikali
na kumtaka mkurugenzi kuendeleza moto wa kuwabana watendaji wake na kuwa wao
kamwe hawatasita kumwajibisha mtu yeyote atakayekwenda kinyume na maadili ya
kazi.
Mkuu wa wilaya Nkasi Idd Hassan Kimanta kwa upande wake aliwataka watendaji hao kuzidisha mshikamano
miongoni mwao na mkurugenzi wao na kuwa siri ya mafanikio ni umoja na kuwa yeye
kama kiongozi wa serikali hatamvumilia mtu atakaepelekea halmashauri hiyo
kudorora na kuharibu sifa nzuri waliyoijenga sasa ya kupata hati safi
No comments