Breaking News

AESHI: WAPUUZENI WANAOSEMA SITOGOMBEA TENA UBUNGE, ATANGAZA RASMI KUGOMBEA TENA!

MBUNGE wa jimbo la Sumbawanga mjini, Aeshi Hilaly ameshangazwa na taarifa zinazoenezwa na baadhi ya wanaCCM wenzake kwamba amejiondoa katika kinyang'anyiro cha kugombea ubunge kwenye jimbo hilo kwa madai ameombwa asigombee na viongozi wa CCM ngazi ya Mkoa  ili kukinusuru chama hicho.

 Akiongea leo katika mikutano ya hadhara kwenye vijiji vya Kankwale na Wipanga, Hilaly alisema kuwa anashangazwa sana na taarifa hizo kwani zinalenga kumpaka matope na kuwapa mwanya wapinzani wake wa  kisiasa walioonyesha nia ya kuchuana nae katika kinyang'anyiro hicho ndani ya CCM.

Hilaly alisema kwamba nia yake ya kugombea ubunge iko pale pale kwa kuwa haoni sababu ya kujiondoa kwani amekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia kupatikana kwa maendeleo endelevu yanayooneka sasa katika jimbo hilo.


"Tumehimiza serikali kutatua kero mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa nishati ya umeme , kimsingi imekwisha sasa tuna umeme wa uhakika, upande wa maji kuna mradi Mkubwa wa Maji wenye thamani zaidi bilioni 30 unatekelezwa na ifika mei mwaka huu Maji yatakuwa sio tatizo tena....


...miundombinu ya barabara imeboreshwa sasa sijui hizi kauli kwamba nisigombee sijafanya lolote zinatoka wapi? alihoji mbunge huyo.

Hata hivyo, wananchi wa vijiji vya Mlanda, Kankwale na Wipanga wamepaza sauti zao wakimtaka mbunge huyo kutothubutu kuiacha nafasi kwani wao wanataka mtu anayefanya kazi inayoonekana na si maneno na porojo za kisomi huku wakishindwa kuwasaidia wananchi kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Mmoja wa wananchi hao, Mathias Pondamali alisema kuwa yeye kwaniaba ya wazee na wananchi wa kijiji cha Wipanga ametoa baraka zote kwa mbunge huyo ili aweze kuchukua fomu na wao kama wazee watamsimamia na kuhakikisha anarudi kuwatumikia tena kama mbunge.

Hata hivyo uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, umebaini kwamba Hilaly ameanza kupigwa zengwe hilo katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoa ambacho kilifanyika hivi karibuni mjini hapa.

Inadaiwa kuwa katika kikao hicho, baadhi ya Viongozi wa CCM wakiongozwa wernyekiti wa CCM mkoa Hypolitus Matete walionyesha msimamo wao wazi kwamba hawapo tayari kumuunga mkono mbunge huyo katika harakati zake hizo.


Inadaiwa kuwa katika kikao hicho kulikuwa na azimio la kutaka Hilaly aombwe kutogombea kabisa ubunge ili CCM iweze kumsimamisha mtu ambaye atakubaliwa na makundi yote yakiwemo ya kidini.

Aidha, Matete akihojiwa kwa njia ya simu kuhusu kusbinikiza Hilaly asigombee nafasi hiyo, alidai kwamba taarifa hizo si za kweli kwani wenye maamuzi ya nani awe mgombea wao ni wanachama wa CCM na vikao husika.

"Wanaofanya maamuzi ni wanachama akipata katika kura za maoni na halmashauri kuu ikarudisha jina lake mie sitokuwa na ujanja..... nitamuunga mkono tu " alisema Matete.

No comments