Breaking News

KILUSWA ATANGAZA KUMVAA AESHI UBUNGE S'WANGA MJINI

Na Gurian Adolf,
 Sumbawanga.

Hatimaye mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Aesh Hilary amepata mpinzani baada ya kada wa siku nyingi mwenye nguvu na ushawishi mkubwa  Anyosisye  Thomas Kiluswa kutangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Akitangaza nia mbele ya waandishi wa habari alisema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kuona miongoni mwa waliotangaza nia mpaka sasa hakuna mtu mwenye dhamira ya kuwawakilisha wananchi.

Alisema kuwa wengi wawaliotangaza nia ni watu ambao hawaishi mjini Sumbawanga wanaishi mikoa ya nje na mji huo ila wamekuwa na mtindo wa kurejea nyakati za uchaguzi na kugombea na wakifanikiwa kupata wanaondoka na kuwaacha wananchi solemba.


Kiluswa alisema kutokana na hali hiyo wamekuwa wakichagua watu ambao hawajui matatizo yao na hivyo kujikuta hakuna msaada kutoka kwa mbunge wao na badala yake wamekuwa na matatizo yale yale miaka yote.


Kada huyo wa CCM alisema kuwa kutokana nayeye kushika nyadhifa kadhaa ndani ya chama hicho na kutumia muda mwingi kuihudumia jamii kwa kujitolea hasa katika Nyanja za elimu na afya ameona sasa umefika wakati wa kuziwasilisha changamoto hizo bungeni yeye mwenyewe kwani atakwenda kuwasemea kitu anachokijua.


‘’kwa muda mrefu nimekuwa nikijitolea katika kutatua changamoto zinazo wakabiri wakazi wa jimbo la Sumbawanga….nazijua vizuri sasa imefika wakati nahitaji mimi mwenyewe kuingia bungeni ili kuwawakilisha wananchi maana nitawasemea kero ninazo zijua’’……alisema.



Aidha alisema kuwa yeye akiwa ni mwanachama wa chama hicho kwa miaka mingi amejijenga vizuri na anakubalika na wapigakura hali ambayo inamuhakikishia ushindi kwani iwapo chama hicho kitampa ridhaa anakubalika hata kwa wapinzani.

Alisema kuwa iwapo atashinda katika kura za maoni hana hofu kuwa atalinyakua jimbo hilo kutokana na vyama vya upinzani kuwa na wagombea dhaifu na kutoungwa mkono na wananchi wengi mkoani humo.


‘’ Naahidi iwapo chama kikinipa ridhaa lazima nitaibuka mshindi kutokana na kuwa ninakubalika ndani na nje ya chama na kutokana na wapinzani kuwa wadhaifu lazima nitapata ushindi na ninakitoa hofu chama changu ushindi ni halali yetu’’…alisema.


Aidha alisema kuwa hivi sasa wanachama wa CCM wanapaswa kuungana na kupambana ili kupata ushindi mkubwa kwani hilo pia litawezekana iwapo chama kitamteua mtu atakayepeperusha bendera ambaye anakubarika kwa makundi yote.

No comments